Ushairi

Ushairi.

USHAIRI
Nitunge kama wakale, walovuma visiwani
Wanituze utotole, kuzindua ya zamani
Walumbi wa zama zile, walitamba kwenye fani
Ushairi ni kipaji, na wala sio kufunzwa

Kiswahili cha wavyele, kilisheheni lahaja
Wahafidhina wa kule, toka Pemba na Unguja
Walijaa semi tele, na kuzipanga kwa hoja
Ushairi ni kipaji, na wala sio kufunzwa

Washaha wa ziwa lile, walizitoa nasaha
Walisifika milele, hawakuwa na fedheha
Walipishwa kwa simile, hawakuweza kuhaha
Ushairi ni kipaji, na wala sio kufunzwa

Tungo zao si kelele, zilijikita kwa dhima
Ziliwafunza wavule, wakaepuka zahama
Hazikuwa tungo tule, zilijaa muadhama
Ushairi ni kipaji, na wala sio kufunzwa

Dhamira ilifikile, kwenye yao mashairi
Tafsida enzi zile, ilitumika dhahiri
Ni tofauti na wale, walokuwa mashuhuri
Ushairi ni kipaji, na wala sio kufunzwa

Mahadhi yalizamile, kwenye andiko husika
Walifikia kilele, kwa lugha wakatajika
Misamiati teule, ilitumika hakika
Ushairi ni kipaji, na wala sio kufunzwa

Wazembwe na wazembwele, nyakanga na nyakanguzi
Wapiga vigelegele, walipiga kwa ujuzi
Majandoni napo pale, hapakuwa waziwazi
Ushairi ni kipaji, na wala sio kufunzwa

Alofunzwa asikile, umalenga ni kipaji
Aloshika ashikile, mie simi mtetaji
Nimekaa kwa mndule, naomba kopo la maji
Ushairi ni kipaji, na wala sio kufunzwa.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close