Ulimi.

ULIMI
Uchunge wako ulimi
Ewe mja nakusia
Kuwa makini na ndimi
Utakuja kuumia
usemayo mara kumi
Kimya ungejikalia
Ulimi hatari sana
Pabaya utatuweka
Ulimi wako uchunge
Kibaya usitamke
Ni bora tu usironge
Kama bubu uoneke
Kuliko fanya mazonge
Na uwe mpeke peke
Ulimi hatari Sana
Pabaya utatuweka
Uchunge ulimi wako
Kutamka yaso mana
Ima kusema mwenzako
Kuzusha vibaya Sana
Tamuudhi mola wako
Tachukia SUBHANA
Ulimi hatari Sana
Pabaya utatuweka
Kabla haujatamka
Lifikiri neno kwanza
Neno nje likitoka
Ni nani litamkwaza
Kama baya kwa hakika
Kitamka litaponza
Ulimi hatari sana
Pabaya utatuweka
Utatuweka motoni
Vibaya kiutumia
Utatuweka peponi
Ukisema yalonia
tumuogope manani
Tusije tukaumia
Ulimi hatari sana
Pabaya utatuweka
Chunga ulimi hakika
Kwani dhima kubwa sana
Maneno yakishatoka
Ndani hayarudi tena
Neno ukishatamka
Kurudi lashindikana
Ulimi hatari sana
Pabaya utatuweka
Na tumuombe manani
Mola wetu SUBHANA
Atukinge na kudhani
Kutamka yasomana
Tutamke ya thamani
Sio ya kusengenyana
Ulimi hatari sana
Pabaya utatuweka
(MTUNZI: BINTRASOOL)