Ushairi

Ujinga si vazi letu.

Ujinga watumaliza, ukweli nawaambia,
Tena unatulegeza, hatuwezi ukimbia,
Tumekumbatia giza, kwa shimo twadidimia,
Ujinga si vazi letu, Tanzania tujivue..

Kuna mda ninawaza, tulipokwamia wapi,
Hatupendi kuuliza, wala kujua ni vipi,
Tupate la kutatiza, hatujui twenda wapi,
Ujinga si vazi letu, Tanzania tujivue..

Umetawala ujinga, ndani ya jamii zetu,
Ninani anayepinga, hatujitambui katu,
Mambo twaungaunga, hatujui haki zetu,
Ujinga si vazi letu, Tanzania tujivue..

Ujinga kwa watawala, wakubwa wadogo pia,
Hatujitambui wala, hatujui fikiria,
Kichafu au jamala, hatuwezi pangilia,
Ujinga si vazi letu, Tanzania tujivue..

Shida ni elimu yetu, au malezi nyumbani,
Au mfumo ni butu, mitaala ya zamani,
Hatuwezi kila kitu, twaishi kihayawani,
Ujinga si vazi letu, Tanzania tujivue…

Ujinga umetujaa, kupenda yasonamana,
Akili zimepumbaa, machafu kila namna,
Mambo maovu hadaa, umbea twapenda sana,
Ujinga si vazi letu, Tanzania tujivue..

Tumejawa na lawama, kusema tusoyajua,
Mahodari wa kusema, hatuwezi kutatua,
Kila siku tupo nyuma, nani atatuinua,
Ujinga si vazi letu, Tanzania tujivue…

Na ujinga ni mtaji, mkubwa wa kisiasa,.
Kupewa unga wa uji, au pombe na anasa
Sahau tekinoloji, na elimu ya kisasa,
Ujinga si vazi letu, Tanzania tujivue..

(Malenga ni Ibn Kimweri)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Check Also

Close
Back to top button
Close
Close