Ushairi

Tubadirike.

Tumeumbwa kwa dhumuni, la kumuabudu Mola /
Hili liwe akilini, kabla mazima kulala /
Uhai sikufitini, maasini ukafula /
Lengo langu uzinduke, pabaya sije ishia ////
*
Usiringe kisa pumzi, uhai huu pumbao /
Watoweka ka ushuzi, katu haunaga ngao /
Mjue vyema Mwenyezi, tambua yake mazao /
Ninakupa za usoni, tabia hiyo badili ////
*
Usiringe kisa cheo, wenzako walishapita /
Waliishi kwa upeo, baraka walizipata /
Kija kosa egemeo, hakika utajajuta /
Ninakupa za usoni, tabia hiyo badili ////
*
Usiringe kisa pesa, si wa kwanza kumiliki /
Kuendekeza anasa, kwenye kosa kweka tiki /
Ipo siku utanasa, tatengwa na halaiki /
Ninakupa za usoni, tabia hiyo badili ////
*
Usiringe kisa mali, wapo wenye zaidiyo /
Wewe kwao upo chali, wakuona kibogoyo /
Sie usitukejeli, na kutuona poyoyo /
Ninakupa za usoni, tabia hiyo badili ////
*
Usiringe kisa siha, tambua kuna maradhi /
Ukijivika ujuha, yupo aneyekuhodhi /
Ukiandaa jeraha, jipange kuomba radhi /
Ninakupa za usoni, tabia hiyo badili ////
*
Usiringe kisa ndoa, siyo wa kwanza kuoa /
Usije kupata doa, utashindwa kukohoa /
Mkeo kimpopoa, kuna fundi wa kung’oa /
Ninakupa za usoni, tabia hiyo badili ////
*
Nane beti nasimama, za uso zituamshe /
Kizazi kiwe salama, nyoyo zetu izikoshe /
Fuadini kuwe kwema, imani ituboreshe /
Lengo langu tuzinduke, pabaya sije ishia ////

(Malenga ni Bin Omary)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close