Ushairi

Sichoke.

USICHOKE
Mie jogoo la shamba, siwezi wika mjini
Nisichanike misamba, bora nibaki nyumbani
Kule mwana sitotamba, matungu yawe moyoni
Ewe akili fikiri, fikiri maisha yangu

Ewe akili fikiri, fikiri maisha yangu
Kesho yangu itabiri, yawate ya walimwengu
Usijeinywa shubiri, dunia ikawa tungu
Miguu nawe tembea, safari bado ni ndefu

Miguu nawe tembea, safari bado ni ndefu
Kamwe usijezembea, wakakuona dhaifu
Mwenzio nakuombea, atakujibu Raufu
Weye chapa zako lapa, karambukia maisha

Weye chapa zako lapa, karambukia maisha
Ila usiwe na pupa, hadhiyo ukajishusha
Ukibwagwa na wa hapa, wakule watakuvusha
Jikaze mwana jikaze, maisha si lelemama

Jikaze mwana jikaze, maisha si lelemama
Kujiuwa usiwaze, hata utakapokwama
Mawazo mawi yapuze, pambania mwisho mwema
Fahamu lolote jema, halikosi maumivu

Fahamu lolote jema, halikosi maumivu
Ushauri wake mama, mwana nisiwe mvivu
Punje ile ya mtama, yahitaji ukomavu
Leo zikubali dhiki, kesho utafarijika

Leo zikubali dhiki, kesho utafarijika
Zingatia itifaki, nawe huko utatoka
Zidi kusaka riziki, na kamwe usijechoka
Hawawezi kuiziba, pengine kucheleweshwa

Hawawezi kuiziba, pengine kucheleweshwa
Kumbuka haba na haba, mwishoni huunganishwa
Zikakijaza kibaba, na sifa kikabebeshwa
Mgaa gaa na upwa, hawezi kula mkavu

(Malenga ni Daniel Wambua).

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close