Ushairi

Shime wakulima.

SHIME WAKULIMA
Mvua kuu inanyesha, wakulima tuamke
Tusipande pantosha, uzembe nauatike
Makonde kuyasafisha, mazao nayapandike
Shime wakulima shime, tujifungeni vibwebwe

Mbegu za kila aina, shambani natuzizike
Majembe yawe wasena, kuchapo natuyashike
Ijapofika mchana, kamwe tusipumzike
Shime wakulima shime, tujifungeni vibwebwe

Mtama nayo mahindi, tuyapande yachipuke
Yapali’we kiufundi, magugu yasiyafike
Tuichungeni milundi, katu isikwaruzike
Shime wakulima shime, tujifungeni vibwebwe

Mpunga upandwe sana, bei dukani ishuke
Vichaga viwe vipana, pomoni navijazike
Mapema visijechina, madukani tukufike
Shime wakulima shime, tujifungeni vibwebwe

Mbogamboga za majani, shambani tuzilimbike
Mchicha nao mwangani, maradhi tuyaepuke
Vibwando tuvithamini, ngozi zitulainike
Shime wakulima shime, tujifungeni vibwebwe

Mihogo natuipande, visamvu navitundike
Kwayo michi tuviponde, kisha nazi tuvipike
Michanyato yazo kunde, tuipike ipikike
Shime wakulima shime, tujifungeni vibwebwe

Isitutoke bidii, muwi njaa atufike
Mvua hino tuitii, kukicha tukarambuke
Tukumbuke nchi hii, kilimo ndo uti wake
Shime wakulima shime, tujifungeni vibwebwe

Pulikani wakulima, maradufu nisikike
Chakula chetu ni sima, asubuhi tuzinduke
Hapa mwisho nasimama, jasho nalisinitoke
Shime wakulima shime, tujifungeni vibwebwe.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close