Ushairi

Shime Lungalunga.

SHIME LUNGALUNGA
Salamu nyingi salamu, nazituma wanagenzi
Nazituma kwa nidhamu, wanafunzi mzienzi
Naichukua kalamu, malenga wenu kipenzi
Shime wana Lungalunga, tufunge vyetu vibwebwe

Kamwe tusitetereke, Mwereni hadi Perani
Na sisi tuelimike, tutambulike nchini
Keshoni tuthaminike, tuingiapo vyuoni
Shime wana Lungalunga, tufunge vyetu vibwebwe

Nyie malaika Mamba, katu msilainike
Mkaja tundikwa mimba, mwishoni muaibike
Wa Ngozi watawachamba, namba wani wawapoke
Shime wana Lungalunga, tufunge vyetu vibwebwe

Lungalunga tuamke, Gugu hata Kikoneni
Mkia tusiushike, matokeo yawe chini
Makwenyeni tudamke, pamoja na Mwashetani
Shime wana lungalunga, tufunge vyetu vibwebwe

Wanafunzi tuzinduke, Shirazi Mwananyamala
Kileleni tukufike, Menzamwenye halahala
Magombani mng’atuke, mzichape zenu ndala
Shime wana lungalunga, tufunge vyetu vibwebwe

Twahitaji wahandisi, manesi na marubani
Wakili na majasusi, walimu na madiwani
Wakae kwenye ofisi, heshima iwasheheni
Shime wana lungalunga, tufunge vyetu vibwebwe

Hapa nafunga uneni, naenda bila kelele
Menzamwenye ndo nyumbani, kijiji cha hapa Kwale
Tukipita mitihani, mie nitawapa dole
Shime wana lungalunga, tufunge vyetu vibwebwe.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close