Ushairi

Shairi la ukaraguni.

Tumekosa Nini?

Mungu muumba dunia, mimea na wanadamu,
Nimekuja nikilia, pasi kujali kaumu,
Wewe ndiwe waridhia, pita nasi hali ngumu,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Kamwe uwezo hatuna, tungeishika dunia,
Tuweze kutakasana, mawele sijeingia,
Na hongo tungepeana, hasa kwa korona pia,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Yarabi tumejifunga, kwa vyumba pasi kutoka,
Hata na hewa kupunga, mekuwa shida hakika,
Halafu kutangatanga, pia imezuilika,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Au wafundisha nini, tuweze kulifahamu,
Magoti tupige chini, kwa toba situhukumu,
Tughofire kwa yakini, kwa korona loharamu,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Woga umetukithiri, toka juu hadi chini,
Twajiogopa si siri, pasi hata walakini,
Fukara na matajiri, hawana matumaini,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Kama ni kukesha pia, nimefika wiki mbili,
Chochote hujanambia, nijue unatujali,
Wana nao wanalia, wachukizwa hii hali,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Tunusuru hili janga, lisije kutumaliza,
Upulike kwetu mwanga, ututoe kwenye giza,
Gizani tutajitenga, tunahitaji mwangaza,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

Kaditama tukupeni, ng’ombe au gari kubwa,
Kafara tukufanyeni, tuweze kukombolewa,
Tulaze matumaini, tusiwe katu watumwa,
Mbona tunaangamia, Mungu tumekosa nini.

(Toney Francis Ondelo
“Chomsky Mswahili”
Ndhiwa-Homabay)

Tags
Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close