Ushairi

Shairi la Maringo ni ya nini.

MARINGO NI YA NINI?


Una damu mishipani, nyekundu kama ya kwangu,
Kuishi u duniani, huishi kwenye mawingu,
Uyaalayo nadhani, ndo tofauti na yangu,
Hayo maringo ya nini, ulonayo hayadumu.

Unywapo chai maziwa, kwangu nile mkandaa,
Sharubati unapewa, nionapo nabung’aa,
Japo hapa napagawa, kila siku ni dagaa,
Hayo maringo ya nini, ulonayo hayadumu.

Mavazi unovalia, yametolewa Japani,
Yanakushika sawia, siyo kama yangu duni,
Matumbani kiingia, bei yangu ishirini,
Hayo maringo ya nini, ulonayo hayadumu.

Yangu duni hudumu, ila yote huzeeka,
Yachanikapo haramu, yatupwa kwenye vichaka,
Mwenzio hana hamu, zote za deki hakika,
Hayo maringo ya nini, ulonayo hayadumu.

Ulivyonunua gari, hatupumui wenziyo,
Mambo kwetu siyo shwari, kwa baraka ulonayo,
Waringa kwa utajiri, mali wengine wanayo,
Hayo maringo ya nini, ulonayo hayadumu.

Twaja huko polepole, huu ndio wetu mwendo,
Mwendo pasi ya kelele, ule wa mema matendo,
Tutafika vilevile, si dharau ni upendo,
Hayo maringo ya nini, ulonayo hayadumu.

Enyi wajawa maringo, twadai tuwie radhi,
Tayari tuna mipango, kupandisha zetu hadhi,
Msijaze zetu bongo, kwa hayo yenu maradhi,
Hayo maringo ya nini, ulonayo hayadumu.

(Toney Francis Ondelo
Chomsky Mswahili/Malenga mjalisiha
Ndhiwa-Homabay)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close