Ushairi

Rais Fungua nchi.

Kwa muda tumenyamaza,lakini tumerejea,
Hata kama twajikaza,ni mengi tumepitia,
Na nyumbani twajilaza,sadirini twaumia,
Rais fungua nchi,tumechoka na nyumbani.

Korona imepungua,na sasa wangoja nini?
Wananchi twashangaa,mikutano hadharani,
Ninakusihi fungua,tusiumie mbeleni,
Rais fungua nchi,tumechoka na nyumbani.

Twaona nazo siasa,wabunge watukanana,
Hawaoni ni makosa,inafaa kuwakana,
Hakuna wa kuwanasa,ukweli kuna korona?
Rais fungua nchi,tumechoka na nyumbani.

Kila siku twakereka,hatuna matumaini,
Ukweli twalalaika,tukiwa huku nyumbani,
Vipi tutasaidika,na shida hizi jamani?
Rais fungua nchi,tumechoka na nyumbani.

Mjini na vijijini,watoto wamepotea,
Tuambie zako plani,za nchi kuifungua,
Twangoja yako idhini,kwa muda ‘mevumilia,
Rais fungua nchi,tumechoka na nyumbani.

Na masharti hakuna,watu wengi hawafati,
Watu wengi twawaona,mikutano hiwapiti,
Kotekote kila kona,wanatupa hatihati,
Rais fungua nchi,tumechoka na nyumbani.

Uketipo ikuluni,jaribu kutafakari,
Pokea yetu maoni,ufungue kwa hiari.
Utilie maanani,hakuna tena hatari,
Rais fungua nchi,tumechoka na nyumbani.

(Lionel Asena Vidonyi-Malenga Kitongojini)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close