Ushairi

Pera limeiva .

*PERA LIMEIVA.*
Ni vipi nitasombera,mti ule wa jirani,
Kulichuma nalo pera,ambalo nalitamani,
Pera kubwa ja mpira,lanivutia usoni,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Natamani kulichuma,lazidi kunivutiya,
Ni nani nitamtuma,aweze kunileteya,
Mbona nijishike tama?Pera nikiliwaziya,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Kila siku naliona,lanifanya kufikiri,
Nami melipenda sana,kulila niko tayari,
Wallahi nitakazana,nilichume kwa kiburi,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Kwa jirani kuna kuta,vipi nitalifikia,
Natamani kulipata,ningali mwenye tamaa,
Nikipata sitajuta,bali nitafurahia,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Kwa muda najilaumu,mbona sina mikakati,
Tajikaza ilhamu,sitaki tena kuketi,
Kwa hivyo tanilazimu,nisipoteze wakati,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Jirani naye mkali,hataki kunisikia,
Vyovyote kwa kila hali,nitazidi kumwambia,
Heri ajue ukweli,kuliko kumuibia,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Jambo lipi nitafanya,na pera laniduwaza,
Mwenyewe amenionya,sitaki kumchokoza,
Na tayari ashamanya,sababu nimemweleza,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

Tamati sasa natua,itabidi kutulia,
Kwa sasa nimeamua,kuweza kumsikia,
Bure nitajililia,mwishowe nitaumia,
Pera nalo limeiva,natamani kulichuma.

(Malenga Kitongojini)

Show More

Related Articles

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close