Riek Machar Apatikana na Korona.

Makamu wa rais wa kwanza wa Sudan kusini ameambukizwa ugonjwa tandavu wa Korona.Imethibitishwa pia mke wake,Angelina Teny,pia amepatikana na ugonjwa huu hatari.

Dkt.Machar alithibitisha habari hizi alipokuwa akizungumza kwenye mazungumzo ya kitelevisheni siku ya Jumatatu.Amesema kuwa wako kwenye karantini katika nyumba yao.

Inadaiwa pia wafanyakazi wa makamu huyo wa rais ikiwemo walinzi wameambukizwa Korona.Hii ni baada ya kutagusana na baadhi ya watu kwenye jopo lililoteuliwa kutafuta mbinu za kupiga vita Korona nchini humo.

Ikumbukwe kuwa Sudan kusini ina watu mia mbili tisini walioambukizwa kufikia sasa.

Aidha, Sudan kusini ndio nchi changa zaidi duniani na imeathirika na vita vya miaka mingi vya kuwania madaraka hasa katika ya Rais Salvakir na makamu wake Machar ila mzozo huu ulitatuliwa.

Mabadiliko Ya Tabia-nchi.

Mabadiliko ya tabia-nchi ni janga la kimataifa ambalo limeathiri maisha ya watu kwenye jamii kiujumla hasa wale wanaoishi mijini.Kupanda kwa nyuzi za joto duniani kumechangia majanga mengine mathalan gharika,ukame n.kHaya mabadiliko yametokana matumizi ya gesi zenye sumu ambayo huachiliwa hewani bila mpango maalum.Athari zake zimedhihirika waziwazi kupitia kuharibika kwa miundomsingi mijini kama vile barabara, sekta ya afya, ukulima n.kShirika la mazingira duniani (U.N.E.P) kupitia ushirikiano na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali inatafuta mbinu za kupunguza makali yake.Ili kushinda janga hili italazimu ushirikiano wa washikadau katika ngazi za kitaifa na kimataifa.Baadhi ya mpango za shirika hili ni uhamasishaji kuhusu mazingira, matumizi nishati zinazoweza kutumika tena, mafunzo ya warsha mbalimbali.Viongozi wa mataifa yenye nguvu duniani walikutana mwaka huu kwenye mkutano wa COP-27 kujadili mipango ya kuhifadhi mazingira.Waliamua kila taifa litoe ngwenje fulani ili kuweza viwanda kutumia nishati zinazoweza kutumika tena.Ingawa mpango huu unakabili na tishio la kutotimizwa kwani mataifa mengine hayajakubali.Ikumbukwe kwamba miji ina nafasi kubwa katika mafanikio ya janga hili.Inasubiriwa kuona kama juhudi zinazofanywa zitafua dafu kwani wanasayansi wameonya kuwa binadamu anakabiliwa na tishio la kuangamia kama tatizo hili halishughulikiwa vilivyo.

Félicien Kabuga Akamatwa.

Mshukiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda, Félicien Kabuga,amekatwa kwenye eneo la Asnières sur Seine ambao ipo kwenye viunga vya mji mkuu,Paris,Ufaransa.Mshukiwa huyu anatuhumiwa kushirikiana na wengine kuwaua takriban watu elfu mia nane wa jamii ya Tutsi mwaka wa 1994.Inadaiwa kuwa ndiye aliyefadhili mauaji ya watu hao kwa kuwalipa watu fulani.Amepatikana baada ya miaka karibu ishirini na sita ambayo alisakwa bila ya mafanikio.Watu mmoja alidhaniwa kuwa alistakimu nchini Kenya na kuwa baadhi ya viongozi walifanya juhudi ili asikamatwe ila serikali ilikana madai hayo.Inadaiwa aliishi huko Paris kwa kutumia jina lisilo la kweli.Kabuga ni mfanyabiashara anayetoka katika kabila la Hutu na ndiye mwasisi wa kituo cha habari cha Radio Télévision Libres des Mille Collines(RTLM) ambayo inadaiwa kuchochea kutafutwa na kuuawa kwa watu wa jamii ya Tutsi.Ikumbukwe mauaji ya kimbari ya Rwanda yalianza baada kufyatuliwa risasi kwa ndege iliyokuwa ikibeba Rais Juvenal Habyarimana na kuwaua wote waliokuwemo.Jambo hili liliibua hisia kinzani baada ya kudaiwa kuwa ikifadhiliwa na waasi wa Tutsi.Inatarajiwa kuwa atafikishwa kwenye mahakama ya kimataifa mjini Hague,Uholanzi kujibu mashtaka ya mauaji na uchochezi.

Chimbuko la Korona.

Suala la ni wapi ugonjwa tandavu wa Korona ulikotokea bado haiyumkiniki kwani limezua mjadala mpevu ulimwenguni kote.Tetesi ziliibuka kwamba huenda virusi hivi hatari vya Korona vilitokea katika maabara moja ya kufanyia utafiti kwenye mji wa Wuhan,China.Haibainiki ni vipi kwani inadaiwa kuwa huenda ilisababishwa na utepetevu wa wa watafiti au ilikuwa tu ajali ya kawaida.Isitoshe,taarifa nyingine inadai kuwa huenda virusi hivi vilitokea kwa popo ambao hatimaye walivisambaza kwa adinasi.Tatizo lilipo kwenye dhana hii ni inawezekana vipi kuwa utagusano wa binadamu na popo ndio uliosababisha janga hili.Ni ukweli usiokanushika kuwa utafiti uliofanywa kwenye baadhi ya wanyama umethibisha kuwa wanaweza kuambukizwa ugonjwa huu hatari.Suala hili tata limesababisha mvutano katika ya nchi ya Amerika na China kwani Marekani inadai kuwa kuna ukweli unaofichwa na China kuhusu chanzo cha ugonjwa huu.Hivi majuzi Rais wa Amerika,Donald Trump,alisema huenda atawatuma maafisa wake wa ujasusi China kubaini kiini cha ugonjwa wa Korona.Aidha,amepunguza ufadhilii kwa shirika la afya duniani (W.H.O) kwa sababu ya kile alichokiita kama upendeleo kwa China.Ingawa shirika hilo muhimu la afya limekana madai hayo na kusema kuwa wakati huu si wa siasa au mengine bali kuangazia afya ya watu ulimwenguni kote.Inasubiriwa kwa udi na uvumba kuona kama ukweli wa chanzo cha ugonjwa huu utabainika ama vuta nikuvute,shutumu nikushutumu ndizo zitazidi.Muhimu zaidi ni kufuata masharti yanazidi kupewa kuzuia maambukizi zaidi mathalan kukaa mbali wa mita moja,kuosha mikono,kuenda hospitalini iwapo unaona una dalili za Korona, kuvaa kitamvua/maski n.k.Pamoja tuangamize Korona!!!!!!

Aina na mbinu za tafsiri.

Tafsiri ya neno kwa neno.
Hii ni tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pwekepweke kwa
kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha wala muundo wala
utamaduni wa lugha lengwa. Mpangilio wa mofimu na maneno wa lugha
chanzi haubadiliki,pia tafsiri hii hulenga tu kupata maana ya kimsingi au ya kamusi. Katika tafsiri hii matini iliyofasiriwa huandikwa chini ya matini ya
lugha chanzi.

Tafsiri sisisi.
Tafsiri hii hutoa maana za kimsingi za maneno yakiwa pwekepweke kwa
kuzingatia kanuni za kisarufi za lugha lengwa hususani sintaksia. Mbinu hii
haizingatii muktadha wala utamaduni wa lugha lengwa.

Tafsiri ya Kisemantiki.

Mbinu hii ya tafsiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa
kufuata sarufi ya lugha lengwa. Tafsiri ya kisemantiki huwekea mkazo kwenye
maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi.

Tafsiri ya Kimawasiliano.
Tafsiri hii inazingatia na kumlenga msomaji wa matini lengwa ambaye
hatarajii kupata ugumu wowote katika matini anayosoma, anatarajia kupata
tafsiri nyepesi ya dhana za kigeni katika utamaduni wa lugha yake.

Tiba Ya Korona Yapatikana.

Wiki jana habari zimeibuka kwa mojawapo ya nchi maskini zaidi katika bara la Afrika limevumbua dawa inayoweza kutibu ugonjwa tandavu wa Korona.Nchi ya Madagascar imezindua dawa ya miti shamba inayoweza kuzuia kwa kiwango kikubwa virusi kuzaana mwilini mwa mgonjwa wa Korona.Rais wa Madagascar,Andry Rajeolina,kwenye mahojiano na kituo cha habari cha ‘Radio France International’ amedai dawa hiyo ina ufanisi mkubwa ikizingatiwa kwamba nchi yake imepata nafuu baada ya wagonjwa mia moja na watano kupona baada ya kuitumia.Ikumbukwe kwamba dawa hiyo inatokana na mti wa ‘Arthemisia’ na imetumiwa hapo awali kutibu magonjwa anuwai kama vile malaria.Hata hivyo, shirika la afya duniani (W.H.O) imeonya vikali dhidi ya matumizi ya dawa za mitishamba ambayo haijafanyiwa utafiti wa kutosha na kuidhinishwa.Ingawaje Rais wa Madagascar amedai kuwa hizo ni porojo za kujaribu kuzuia matumizi yake.

Aina za Tafsiri.

Aina za tafsiri za tafsiri ni kama zifuatazo:

 1. Tafsiri ya fasihi
 2. Tafsiri ya riwaya
 3. Tafsiri ya tamthiliya
 4. Tafsiri ya ushairi
 5. Tofauti ya tafsiri za kifasihi na zisizo za kifasihi.

Tafsiri za matini za kisayansi/kiufundi.

Matini za kisayansi au za kiufundi ni zile matini zinazotumia msamiati
maalum, mfano matini za tiba, uhandisi, elektroniki, sayansi ya kompyuta na
sayansi nyinginezo. Tafsiri ya matini hizi haijiegemezi katika utamaduni
wowote na hutofautiana na tafsiri nyingine kutokana na matumizi makubwa ya
istilahi. Matini za kiufundi pia hutumia picha, grafu, michoro, vielelezo,
takwimu n.k na huandikwa katika umbo la ripoti ya kiufundi. Mfasiri
anapofasiri matini hizi hukumbana na zoezi la uundaji wa istilahi mpya
kutokana na kukosa visawe vya istilahi za lugha chanzi katika lugha lengwa.

Tafsiri na utamaduni.
Lugha ni kipengele cha utamaduni wa jamii, pia lugha inatumika kuelezea
utamaduni wa jamii husika. Maana za maneno katika lugha hujengwa kutokana
na utamaduni wa jamii inamozungumzwa lugha hiyo. Hivyo tafsiri siyo tu
mchakato wa kiisimu, bali pia ni mchakato unaojumuisha masuala yanayohusu
utamaduni wa wazungumzaji wa lugha husika. Tofauti za kiutamaduni baina
ya lugha chanzi na lugha lengwa ndizo zinampatia mfasiri matatizo makubwa
wakati wa kufasiri, mathalani mfasiri anapofasiri lugha ya Kiingereza na lugha
ya Kiswahili. Vipengele vya kiutamaduni vinavyoweza kuleta ugumu katika
kufasiri ni kama nguo, vinywaji, violwa, ekolojia, siasa na dini.

Tafsiri ya mashine na tafsiri ya binadamu.
Mchakato wa kufasiri huweza kufanywa na binadamu au mashine. Mchakato
wa kufasiri kwa kutumia mashine umekuja kutokana na maendeleo ya sayansi
na tekonolojia ambapo badala ya binadamu kutumia maarifa yake zipo mashine ambazo zinaweza kufanya kazi hiyo.

Uhusiano baina ya tafsiri na lugha.

Taaluma ya tafsiri ni taaluma kama taaluma nyingine ambazo haziwezi
kujitegemea bila kuhusiana na taaluma nyingine. Kama mwili wa mwanadamu
unavyofanyakazi ambapo viungo vyake vyote vinategemeana katika
kukamilisha majukumu ya kuona, kutembea, kula, kulala, kuongea n.k.
Taaluma hii ya tafsiri ina uhusiano mkubwa na taaluma nyingine kama:
o Ukalimani
Tafsiri ni uhawilishaji wa mawazo yaliyo katika maandishi kutoka
lugha moja hadi nyingine. Ukalimani ni uhawilishaji wa ujumbe au
mawazo ulioko katika mazungumzo kutoka lugha moja hadi nyingine.
o Isimu linganishi
Isimu linganishi ni tawi la isimu linalofanya uchanganuzi wa lugha
mbili au zaidi ili kuzilinganisha na kuzilinganua. Taaluma hii
humsaidia mfasiri kuelewa mifumo ya lugha chanzi na lugha lengwa na
namna zinavyotumia zana zake za kiisimu kutolea taarifa mbalimbali.
o Isimu jamii
Ni taaaluma inayochunguza uhusiano wa lugha na jamii inayotumia
lugha hiyo. Wakati wa kufasiri mfasiri hanabudi kuzingatia uhusiano
huu ili aweze kufanya tafsiri sahihi na bora.
o Isimu maana
Isimu maana ni tawi la isimu linaloshughulikia maana za maneno na
tungo katika lugha. Katika taaluma hii mfasiri huweza kujua maana za maneno au tungo na kujua maana hizo hazitokani katika maneno pweke pweke bali namna yalivyotumika muktadha mahsusi.

Elimu Mtindo.
Ni taaluma inayojishughulisha na uainishaji wa mitindo ya lugha na
miktadha ya matumizi yake. Taaluma hii humwezesha mfasiri
kubainisha mtindo wa matini chasili ili auhawilishe katika matini
lengwa.

Isimu amali.
Ni taaluma inayochunguza amali na desturi za jamii fulani na namna
zinavyathiri matumizi ya lugha. Mfasiri yampasa kufahamu amali na
desturi za jamii zinazotumia lugha zinazofasiriwa.

Mawasiliano
Mawasiliano ni uhawilishaji na utambuzi wa maana katika jamii moja
na nyingine kwa kutumia lugha. Kwa kuwa lengo la tafsiri ni
kuziwezesha jamii mbalimbali kuwasiliana, mfasiri hana budi kipata
taaluma hii kwa kina.

Uundaji wa Istilahi
Ni taaluma inayochunguza mbinu mbalimbali za uundaji wa istilahi,
kwa kutumia mbinu hizo mfasiri anauwezo wa kuunda istilahi pale
anapokosa visawe katika lugha lengwa.

Mantiki.
Ni taaluma inayochunguza usahihi au ukweli wa matini chanzi kabla ya
uhawilishaji wake. Hivyo kauli zinazokanganya hurekebishwa kabla ya
kutafsiri ili kujiepusha na kutafsiri uongo.

Isimu Kokotozi.

Ni tawi la isimu linalojishughulikia takwimu na kanuni za kufinyanga
lugha kwa mtazamo mkokotoo. Taaluma hii inajihusisha na tafsiri
kupitia matumizi ya mashine na tarakilishi katika kuhawilisha ujumbe
kutoka lugha chanzi hadi lugha lengwa.

Isimu Tumizi
Ni taaluma inayochunguza matumizi ya lugha kwa lengo la kubainisha
na kutoa suluhu kwa matatizo yanayojitokeza. Taaluma hii ni muhimu
kwa mfasiri kwani mfasiri hujihusisha na uamilifu wa lugha katika
matumizi.

Isimu Razini.

Isimu razini ni taaluma inayochunguza mchango wa akili
unaomuwezesha binaadamu kupata, kutumia, kuelewa na kuzalisha
lugha. Taaluma hii inajihusisha na tafsiri kwani katika zoezi la kuelewa

Sifa za Fonimu.

Fonimu ina sifa zifuatazo:

 1. Kila fonimu ina sifa zake za kifonolojia zinazoonesha uamilifu wa fonimu hiyo katika lugha maalumu.
 2. Kila fonimu hushiriki kikamilifu katika ujenzi wa maneno na kutofautisha maneno yenyewe.
 3. Fonimu moja haina maana kwa kuwa si kiashiria cha kiashiriwa chochote.
 4. Ukibadili fonimu moja katika neno basi maana ya neno hilo itabadilika.
 5. Kila fonimu ina sifa zake za kifonetiki zinazoweza kuelezwa na kufafanua fonimu hiyo.
 6. Kila lugha ina fonimu zake na fonimu hizo hazifanani katika uamilifu wake.
 7. Ukipunguza fonimu katika neno maana ya neno hilo itabadilika au kupotea kabisa.
 8. Ukipangua mpangilio wa fonimu katika neno maana ya neno hilo itabadilika au kupotea.
 9. Ukiongeza fonimu katika neno maana ya neno hilo itabadilika au kupotea.
 10. Sifa zote za fonimu za lugha maalum huelezwa na watumiaji wa lugha hiyo ikiwa ni sehemu ya umilisi wa lugha yao.

Matawi Ya Isimu.

Isimu-ubongo– ni tawi la isimu linalochunguza mahusiano kati ya lugha na
michakato ya kiakili (ubongo), uzalishaji wa matamshi katika ujifunzaji wa lugha.
Msingi mkubwa katika tawi hili la isimu ni kuwa mchakato wa uzungumzaji
huanzia katika akili ya mtu. Hivyo mwanaisimu ubongo hujaribu kutafitina kueleza
ni nini hasa kinatokea katika ubongo ambacho kinamwezesha mwanadamu
kuzungumza. Pia hutafiti na kueleza matatizo katika lugha yanayotokana na
matatizo katika ubongo wa mwanadamu.
Isimujamii – Isimu Jamii (social linguistcs) – ni tawi la isimu (elimu ya lugha)
linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano baina yake.
Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti; aina mbali mbali
za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii
inayoitumia. King’ei (2010), anaeleza kuwa, kwanza lugha ni zao la jamii, na ni
kipengele muhimu sana cha utamaduni wa jamii husika. Pili, lugha hutumiwa na
jamii kuhifadhi amali na utamaduni wake na hasa kama chombo maalumu cha
kuwezesha wanajamii kuwasiliana. Hivyo isimu jamii hueleza na kufafanua
mahusiano ya karibu kati ya lugha na jamii ambayo ndiyo mama wa lugha.
Isimu -anthropolojia– tawi hili la isimu hukijita katika kutafiti na kueleza historia
ya na miundo ya lugha ambazo bado hazijaandikwa.
Isimu- kompyuta – huchunguza matumizi ya kompyuta katika kuchakata na
kuzalisha lugha ya mwanadamu. Ni tawi ambalo kwa hakika si la muda mrefu na
linatokana na maendeleo ya sayansi na tekinolojia hasa baada ya uvumbuzi wa
kifaa kama kompyuta.Isimu-tumizi– huchambua na kueleza matumizi ya nadharia mbali mbali za lugha na maelezo ya kufundishia lugha.(Mr.Simile.O. Utangulizi wa lugha na isimu,Mzumbe University,2012/2013)

%d bloggers like this: