Mashairi ya Kiswahili.

………… MWALIMU NAANGAMIA ……….
mwalimu ninalilia, machozi yatiririka
Serikali saidia, mwalimu ninateseka
Nani atanikwamua, majanga yameniteka
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Mbona ninasahaulika, mwelekezi wa shuleni
Bunge sijatambulika, wakiwepo kikaoni
Wabunge mnanizika, ninaenda kaburini
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Tufanyapo mtihani, mwalimu ninasifika
Nizamapo taabuni, jamii inanizika
Niende wapi jamani, nchi imenigeuka
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Mwajiri niliamini, sasa amenigeuka
Ninakoishi nyumbani, mwenyewe akasirika
Nilikokopa dukani, kooni amenifika
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Enyi nilowachagua, njooni mniauni
Kura niliwapigia, mnitoe taabuni
Nyote mmenipotea, sijawaona machoni
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Kenyatta nilichagua, kwenye seneti Malala
Tindi nilimpigia, tangu aliposimama
Siaya ninatokea, Rasanga niliungama
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Nawalilia wazazi, ninaowafundishia
Nimesema tangu juzi, ombi kunisaidia
Sina pato wala kazi, nyinyi nawategemea
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Maulana nijalie, na cha kutia tumboni
Nani nikamlilie, kama si wewe Manani
Sin’ache niangamie, nilivyofanywa nchini
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Walokuwa marafiki, kitambo walinitenga
Nimebaki kwenye dhiki, Rabana ananichunga
Kubembeleza sichoki, kwa maombi nitafunga
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Kwa kweli sina hakika, nitarejea shuleni
Huenda yakanifika, yanitue kaburini
Iwapo yatatumika, nchi yangu buriani
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo
WALIMU IPO SIKU. KILA MARA WANATUTIA MOYO KUWA NI MUNGU AWEZAYE KUTULIPA. HATIMAYE KAULI HII IMETIMIA. HATUNA WA KUTULIPA DUNIANI. TUNATARAJIA SAA YA MUNGU. Mwalimu Sammy nimelitunga shairi hili si kujisifu kwa vikombe nilivyoshindia shule mbalimbali, si kusifia utunzi wangu wa mashairi bali kuwasilisha vilio vyetu kwa amina. IPO SIKU.
#SavePrivateandBOMTeachers
CC Citizen TV Kenya
#StateHouseKenya
#NTV
KUTV – Mawimbi ya Lugha

Dhana ya silabi.

Jumanne, (2014) Silabi ni kipashio cha kifonolojia kinachohusu matamshi ambacho kwacho sauti za lugha hutamkwa mara moja na kwa pamoja kama fungu moja la sauti.

Feng Shengli, (2003) Silabi ni mpangilio wa fungu la sauti za kutamkwa.

David Crystal, (2003) Silabi ni sauti moja au zaidi inayowakilisha kifungu kimoja cha sauti katika lugha.

Massamba na wenzake, (2004) Silabi ni sehemu ya neno ambayo huweza kutamkwa mara moja na kwa pamoja kama fungu moja la sauti. Maelezo haya yanamaana kwamba maneno ya lugha hutamkwa katika utaratibu wa kufuata silabi.

Kamusi ya Kiswahili sanifu (Toleo la pili, 2004-2005) Inasema kuwa silabi ni sehemu ya neno inayoundwa na konsonanti na irabu au irabu peke yake na kutamkwa kwa pamoja kama fungu moja la sauti. Kwa mfano, “i” na “ta” katika neno “ita” ni silabi mbili tofauti.

Hivyo basi kwa kuangalia maana zilizotolewa na wataalamu mbalimbali tunaweza kuhitimisha kwa kusema kuwa, silabi ni kipashio cha kifonolojia ambacho sauti au fungu la sauti linalojitosheleza kimatamshi, ambacho hutamkwa mara moja na kwa pamoja.

AINA ZA SILABI.
Kwa mujibu wa Massamba (2004), kuna aina mbili za silabi ambazo ni;
Silabi huru.
Silabi funge.

SILABI HURU.
Ni silabi ambazo huishia na irabu. Kwa mfano silabi hizo ni “ka, da, ba, cha na nyingine nyingi. Kimsingi maneno yote ya lugha ya Kiswahili sanifu ambayo yana asili ya kibantu huundwa kwa silabi huru.

Kwa mfano:

 • Mawio-ma-wi-o
 • Kuku-ku-ku

Siku ya mazingira duniani.

Siku ya mazingira duniani huadhimishwa kila mwaka juni 7 ili kuangazia hatua ambayo jamii ya kimataifa imepiga kutunza mazingira.Chakula tunayokula,maji tunayoyanywa,hewa tunayopumua na mengine mengi yanatoka kwenye mandhari yetu.Mwaka huu wa 2020 tunaangazia hatua madhubuti dhidi ya uchafuzi wa mazingira kwani mandhari yetu yashaanza kutupa ujumbe kuwa tusipohadhari tutaangamia.Ili kujilinda lazima kwa vyovyote vile tulinde mazingira.Huu ndio wakati mwafaka kuamka kutoka usingizi wa pono na kupaza sauti kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.Mwaka huu kauli mbiu ni binadamu na dunia.Kama njia moja ya kuhakikisha mafanikio ya kutunza,nchi nyingi duniani zimeafikiana kutupilia mbali matumizi ya gesi chafu kufikia mwaka 2050.Kampuni nyingi tu zimekubali hii hatua.Ikumbukwe maadhimisho haya yanakuja wakati ambapo duniani unakabiliana na mabadiliko ya tabia-nchi.

Dhana Ya Fasihi.

Fasihi kwa ujumla wake ni sanaa ya kutumia lugha ili kuwakilisha wazo fulani kwa hadhira kusudiwa. Hivyo tunaposema kuwa fasihi ni sanaa ya lugha inamaana kuwa fasihi huipamba lugha ya kawaida kuonekana isiyo ya kawaida ili kuwavutia watu na kuwakosha kihisia (Samweli, 2015). Fasihi imegawanyika katika tanzu kuu mbili, ambazo ni fasihi simulizi na fasihi andishi, Kazi hii itajikita hasa katika fasihi simulizi.
Fasihi sumulizi kama utanzu wa fasihi ulianza tangu kuwepo kwa mwanadamu. Mwanadamu asingeweza kuishi vyema katika mazingira yake kijamii bila kuwasiliana, na ili kuwasiliana alihitaji lugha. Lugha ilitumika pia katika maburudisho mbalimbali na huo ndio ukawa mwanzo wa fasihi pia. HIvyo utanzu huu wa fasihi ulianza tangu kuwepo kwa mwanadamu. Utanzu huu hutumia lugha ya masimulizi katika kufikisha ujumbe wake kwa hadhira iliyokusudiwa. Kwa hali hii basi Fasihi simulizi ni utanzu wa fasihi utumiao lugha ya masimulizi yamdomo kujikamilisha kidhima (Mnenuka, 2011).

Uainisho wa tanzu za fasihi simulizi na vipera vyake umezungukwa na utata mkubwa. Uainishaji wa tanzu za fasihi simulizi umekuwa moja ya mambo magumusana katika fasihi hiyo. Ugumu wa uainishaji wa tanzu hizo hutokana na mambo kadhaa. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na yafuatayo;
Kuna vigezo vingi vinavyoweza kutumika katika uainishaji wa tanzu hizo. Vigezo hivi hutofautiana kutoka mwanazuoni mmoja hadi mwingine. Mfano wengine husema kuwa uainishaji huangalia umbile na tabia, na wengine huangalia majina ya tanzu na miundo yake.
Pia tanzu za fasihi simulizi ni nyingi na hutofautiana kati ya jamii na jamii. Kila jamii ina tanzu zake za fasihi simulizi ambazo zinaweza kuwa tofauti na tanzu za jamii nyingine. Inawezekana tanzu Fulani ikawepo katika jamii Fulani lakini isiwepo katika jamii nyingine au inaweza kuwepo lakini ikawa na tabia tofauti kabisa. Mfano katika jamii ya wasukuma na wahaya kuna majigambo ya wanawake (Samweli, 2015).
Tanzu hizo huingiliana, katika fasihi simulizi ni kawaida kwa tanzu kuingiliana, mfano methali huweza kuwa hadithi na hadithi kuwa methali. Hivyo, huwa vigumu kuiainisha tanzu hiyo.
Tanzu za fasihi simulizi hubadilika badilika kutegemeana na muktadha wa utendaji na wakati. Tanzu mpya huweza kuibuka na za zamani kufa. Hivyo ni vigumu kueleza kuna tanzu ngapi za fasihi simulizi labda pia itajwe uainishaji huo ni kwa wakati gani. Mfano utanzu wa nyimbo na kipera cha majigambo ya bongo freva liokuja miaka ya 1980 na kuendelea na kabla ya hapo haukuwepo.
Tanzu na vipera vya fasihi simulizi ni nyingi mno. Tofauti na fasihi andishi yenye tanzu na vipera vichache. Muda mrefu unahitajika kuzitafiti na kuziainisha kwa usahihi katika jamii mbalimbali za Kiafrika.

Mashairi kuhusu Korona.

Navalia barakoa,sokoni mie niende.
Yeye aliyoifua,safii bila ya mende.
Nilikuwa ‘mevalia,alipoifua Sinde
Korona mharibifu,ni lini utaondoka?

Madukani nifikapo,mita mbili wa’nekana.
Madukani wakaapo, usoni zaonekana.
Watu wote waendapo, barokoa waziona.
Korona mharibifu, ni lini utaondoka?

Unawadia wakati, kafiu hili kuanza.
Waondolewa kwa viti, karibuni litaanza.
Naye kukalia siti,taka safari kianza.
Korona mharibifu,ni lini utaondoka?

Askari nao waja,bila hata kukawia.
Saa moja imekuja,wakati wa kuishia.
Wengi awa ni wateja,onekana kulegea.
Korona mharibifu, ni lini utaondoka?

Nyumbani mie nafika,runinga nafungulia.
Ninanyo yaona kaka,korona mewazidia.
Waonekana na shaka,korona inaenea.
Korona mharibifu, ni lini utaondoka?

Chozi lanitoka mimi,niandikapo shairi.
Hataa ha¹liungami,yanitoka tiritiri!
Uchungu onja ulimi,ninapo hili kariri.
Korona mharibifu,ni lini utaondoka?

Ninakuomba Jalali, korona isitupate.
Janga la uchina hili,liache kuwa na kite.
Yaende haya makali, yasiweze ‘nea kote.
Korona mharibifu,ni lini utaondoka?

(Mwalimu Bosire Daniel
Bosiredaniel12@gmail.com)

Jinsi baadhi ya nchi zinavyojitahidi kukabiliana na mabadiliko ya tabia-nchi.

Nchi tofauti duniani zinaendelea kuweka mikakati bomba ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia-nchi ambayo imeathiri sekta mbalimbali hivyo kuchangia kudorora kwa uchumi na mazingira.

Baadhi ya mikakati ni pamoja na upanzi wa miti, uhamasishaji wa umma kuhusu umuhimu wa mazingira safi, kuhimiza watu kukuza mimea kwa kutumia mbolea zinazotokana na wanyama n.k

Nchini Kenya,Rais Uhuru Kenyatta alitoa amri ya kupiga marufuku matumizi ya karatasi ya plastiki.Sheria ilishaanza kutekelezwa na iwapo utapatikana utapigwa faini.

Nchi za umoja wa Ulaya kama vile Ufaransa,Wingereza, Uhispania,Italia, Ujerumani zilifanya mkutano wa kujadili mipango ya kuhifadhi mazingira na kukabili janga hili kiujumla.Baadhi ya maafikiano ni pamoja na mchango wa fedha ili kufadhili viwanda mbalimbali kutumia gesi na nishati zisizoweza kuchafua mazingira.

Nchini Australia binti mmoja wa takriban miaka kumi na sita alianza mpango wa kuhamasisha vijana juu ya athari za janga hili na kushinikiza jumuiya ya kimataifa kuweka mipango madhubuti ya kupunguza madhara zaidi zinazoweza kujitokeza na janga ili.

Ikumbukwe kwamba wanasayansi wameonya kwamba huenda kukashuhudiwa ongezeko la majangwa duniani na ukosefu wa rutuba katika ardhi nyingi kufikia mwaka 2030

Mabadiliko Ya Tabia-nchi: Upanzi wa miti.

Miti ina umuhimu mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia-nchi.Karne ya ishirini na moja imeshuhudia uharibifu mkubwa wa mazingira.Binadamu anazidi kukata miti ovyo bila mpangilio mwafaka na kugeuza misitu makazi yake.Kwenye rubaa za kimataifa tumeona mwaka huu misitu mikubwa ambayo ni vyanzo vya maji duniani vikichomwa na hatua madhubuti kukosa kuchukuliwa.Mfano mzuri ni msitu wa Amazon ambao uko Brazil ulioteketea pakubwa.Imelazimu nchi tajiri duniani kuchanga fedha za kuijenga upya.Nchi Kenya tumeshuhudia vuta nikuvute kati ya serikali na wananchi waliokuwa wakistakimu kwenye msitu wa Mau baada ya serikali kuanza mpango wa kufurusha wananchi waliokuwa wakiishi hapo.Hata wanasiasa wamesikika wakipinga vikali mpango huo.Msitu huo ambao ndio chanzo cha mito mingi nchini humo umeharibiwa sana na kuchangia ukame.Miti ina umuhimu mwingi sana hasa ikizingatiwa kwamba husafisha hewa na kuondoa uchafu uliomo.Aidha,miti huzuia mmonyoko wa udongo ambao umeathiri pakubwa uzalishaji wa vyakula kwani ardhi imekosa rutuba.Miti pia ni makazi ya wanyama mathalan ndege ambao pia huweza kuwa kivutio cha watalii.Miti mingine hutumika kama dawa kwa kutibu magonjwa.Hivyo inalazimu jamii ya kimataifa kufikiria upya mpango mingine kama vile kuchipuka kwa miji na kulinda mazingira kuepusha madhara yanayoweza kupata binadamu.Ikumbukwe kwamba karne ya ishirini na moja imeshuhudia ongezeko la madhara ya kimazingira kama vile mafuriko,ukame,mitetemeko ya ardhi n.k

Historia Ya Mwendazake Prof.Ken Walibora.

Marehemu Ken Walibora Waliaula alizaliwa kati ya mwaka 1964 na 1965,januari sita katika eneo LA Baraki kaunti ya Bungoma kama kitinda mimba.Yeye pamoja na familia yake walihamia eneo la Cherenganyi,kitale,Kaunti ya Tans nzoia.Katika umri wa miaka sita,Walibora aligundua kuwa na majina mawili,Kennedy na George ila akalichagua Kennedy kutokana na umaarufu wa rais wa Marekani wakati huo John F.Kennedy.Masomo
Mwanga wa masomo ya mwenda zake ulitokea chuo cha Nairobi alikojipatia shahada ya first class katika sanaa ya fasihi na Kiswahili Mei 2004.Alijipatia shahada ya uzamili yani masters katika chuo cha Ohio nchini Marekani mwaka 2006.Aliendeleza masomo yake chuoni humo na kujipatia shahada ya uzamifu yani PhD mwaka 2009.Kazi
Marehemu ashawahi fanya kazi kwingi kama mhadhiri,mwalimu,mtangazaji,mwandishi na mchapishajiKati ya mwaka 2005-2007 Walibora alifunza chuo cha Ohio nchini Marekani
Kati ya mwaka 1999-2004 Ken alikuwa msomaji wa habari za kiswahili katika runinga ya NTV
Mwaka 1996-1999 Walibora alifanya kazi kama mtangazaji wa Redio,mhariri na mkalimani katika idha ya KBC
Mwaka 1985-86 Ken alifanya kazi katika wizara ya maswala ya ndani ya nchi
Na mwaka 1988-1996 Marehemu alifunza shule ya sekondari kama mwalimu wa kiingereza na na Kiswahili.Uandishi
Profesa Ken amejishindia tuzo maridhawa kutokana na kazi yake ya uandishiMwaka 2015 marehemu alijishindia tuzo tatu mtawalia za Jomo Kenyatta Literature Prize kufuatia vitabu vyake vya Ndoto ya Amerika,Kisasi Hapana na Nasikia sauti ya mamaMarehemu amejipa sifa kutokana na uandishi wake uliokosha wengi,uchapishaji na uhariri vyote ambavyo amefanya kwingi.Baadhi ya vitabu alivyoviandika na kuchapisha ni pamoja na;
Kidagaa kimemwozea kilichotahiniwa nchi nzima kati ya mwaka 2014-2017.Ken alikiandika kitabu hiki mwaka 2012.
Siku Njema,tungo alilolitunga mwaka 1996.Kitabu hiki ndicho kilichomtambulisha Marehemu katika ulimwengu wa uandishi.
Innocence Long Lost,tungo alilodhihirishia ulimwengu kuwa hakukipenda tu kiswahili pekee bali pia kiingereza
Ndoto ya Amerika 2003
Kisasi Hapana 2009
Nasikia sauti ya mama 2015 na tungo zingine nyingi kama Damu nyeusi na hadithi nyinginezo alichoshirikiana na Ahmed Said Mohamed na Nizikeni papa hapa tungo ndani ya kitabu tumbo lisiloshiba.Hadi kufa kwake Marehemu amekuwa mhadhiri katika Chuo cha Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia cha Riara.Marehemu katika Maisha yake hapa Duniani amesisimua wengi,amefunza na kuelimisha kupitia tungo zake…

Jinsi mabadiliko ya tabia-nchi imeathiri Kilimo.

Mabadiliko ya tabia-nchi yameathiri pakubwa sekta ya kilimo na inatabiriwa kuwa kutaathiri utoshelezi wa vyakula siku za halafu.Utoshelezi wa vyakula duniani unategemea uzalishaji wa vyakula vyenyewe pamoja na upatikanaji wazo.Mabadiliko haya yataathiri utoshelezi wa vyakula madhali bei ya vyakula itakuwa ghali hivyo kuathiri upatikanaji wa vyakula.Maji yanayohitajika katika uzalishaji wa vyakula yatakuwa kidogo sana kwa sababu ya ukame na kupanda kwa matumizi yake katika ukuzaji wa mimea.Aidha, kutakuwepo na mashindano katika kupata ardhi ya kufanyia ukulima kwa kuwa ardhi nyingi zitaendelea kupoteza rutuba hivyo kutokuwa mahali pazuri pa upanzi.Kuongezeka kwa mabadiliko ya hali ya hewa kutachangia kupanda kwa mafuriko,ukame hivyo kuchangia kupanda kwa gharama ya maisha.Licha ya kuwa kupanda kwa halijoto na ongezeko la hewa ya kabondioksaidi kunaweza kusababisha ongezeko la mazao, ni kweli kwamba joto na ukame unaathiri mimea wakati wa kutoa maua.Kuongezeka kwa halijoto duniani pia kumewatatiza wanyama wanaoishi ardhini na majini kwa hawapati chakula na maji yanayowatosheleza.Ongezeko hili la joto pia linachangia kuongezeka kwa viini vinavyosababisha magonjwa.Ongezeko la joto pia linachangia kuongezeka kwa mvua hivyo kusababisha mafuriko inayoharibu miundomsingi na nyumba za watu.Ni muhimu jumuiya ya kimataifa kuelewa athari ya mabadiliko ya tabia-nchi kwa zaraa na kuchukua hatua madhubuti ya kukinga jamii dhidi ya ukosefu wa vyakula hivyo kuhatarisha maisha ya watu.

Athari za mabadiliko ya tabia-nchi.

Mabadiliko ya tabia-nchi imeathiri pakubwa mazingira na binadamu kwa ujumla.Kupanda kwa halijoto duniani kumechangiwa na ongezeko la mkusanyiko wa gesi za kivungulio na kutosawazishwa kwa nishati za duniani.Baadhi ya athari ya mabadiliko ya tabia-nchi za moja kwa moja ni kama vile:

 1. Kupanda kwa halijoto
 2. Kupanda kwa usawa wa bahari
 3. Kushuka kwa barafuto
 4. Kubomoka kwa kiboreshaji
 5. Ongezeko la mvua ya mawe
 6. Kupanda kwa halijoto ya bahari

Mabadiliko ya tabia-nchi zisizo za moja kwa moja ni kama vile:

 1. Ongezeko la ukosefu wa maji na njaa duniani
 2. Kudhoofika kwa watu kiafya kwani kuna magonjwa kama saratani ya ngozi yaliyozuka kwa sababu ya kupanda kwa joto.
 3. Ongezeko la viini vinavyosababisha magonjwa
 4. Ongezeko la hitaji la pesa ili kukabili mabadiliko ya tabia-nchi kwa binadamu.
 5. Kupotea kwa usawazishaji wa kimazingira kutokana na kuzuiwa kwa ongezeko la flora na fauna.
 6. Mabadiliko katika sekta ya zaraa na miundomsingi.

Ikumbukwe athari hizi ni kwa binadamu.#Tukabili mabadiliko ya tabia-nchi.

%d bloggers like this: