Ushairi

Njoo maneno.

NJOO MANENO
Nayatafuta maneno, maneno tena matamu
Nichakate michuano, michuano yakiamu
Narambaza kwa rukono, rukono ‘siwe dhalimu
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Njoo leo nijisifu, nijisifu kwa utunzi
Bora yasiwe machafu, machafu kama ja nzi
Misamiati nyoofu, nyoofu kama ya tenzi
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Natamani kusifika, kusifika kama wale
Muwala ujekuwaka, ujekuwaka kikale
Karabini naishika, naishika kwa vidole
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Ndoto yangu niwakanye, niwakanye wayaate
Maaswi wasiyafanye, wasiyafanye wajute
Chuki zisiwatawanye, zisiwatawanye kote
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Njoo mie narudia, narudia tena sana
Ukija nitawambia, nitawambia kwa kina
Wengi wakishuhudia, ‘shuhudia ya bayana
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Niwafunze wanandoa, wanandoa wasiyumbe
Niyasafishe madoa, madoa yao wapambe
Mazuri kuyadondoa, kuyadondoa mjumbe
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Nakwita niwachekeshe, niwachekeshe wacheke
Tungo zangu ziwe sheshe, sheshe tena zisifike
Zisijezuwa kasheshe, kasheshe zinifunike
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Tungo zile za mahaba, mahaba wenyewe wale
Niwalenge kwayo shaba, shaba ziwafike kule
Kooni zijewakaba, zijewakaba wawele
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Niwakataze wahuni, wahuni wa mitaani
Walevi waso na dini, dini wasoithamini
Watafunaji majani, majani ya hayawani
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie

Njoo maneno mwenzangu, mwenzangu nakuarifu
Fanya hima kaka yangu, kaka yangu mzoefu
Hapa mwisho nenda zangu, nenda zangu pasi hofu
Maneno njoo nakwita, nakwita wanisikie.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close