Ushairi

Nipende nani?

NIPENDE NANI?
Moyo kweli watamani, vya asali na maziwa
Vipo vingi mitaani, hata salamu napewa
Yaliyomo akilini, ndo yanayonizuzuwa
Mwenzenu mie napenda, tatizo nipende nani?

Weupe nawatamani, na gharama siziwezi
Kutunza sio utani, uhawinde kizuizi
Lazima niwe makini, haswa kwenye uchambuzi
Mwenzenu mie napenda, tatizo nipende nani?

Hata kina mwafulani, wanaringa tena sana
Vipicha mitandaoni, tabia wamezichana
Mavazi ya uzunguni, yananichanganya sana
Mwenzenu mie napenda, tatizo nipende nani?

Uzuri si manukato, hayo mambo ya zamani
Nyuso zitele michoto, nywele za Ughaibuni
Sasa kama huna pato, utapendwa kweli Dani?
Mwenzenu mie napenda, tatizo nipende nani?

Nilimwomba tu nambari, na akaniomba mia
Nikaikwepa hatari, hakujuwa natania
Jumbe zake furifuri, kwangu aling’ang’ania
Mwenzenu mie napenda, tatizo nipende nani?

Warembo wenye miwani, kuna jambo nalishuku
Siweki paruwanjani, nikaambiwa na chuku
Naliachia gizani, mbaki na dukuduku
Mwenzenu mie napenda, tatizo nipende nani?

Bora mapenzi ya Allah, kwa wale wanipendao
Haya hayataki hela, wala si ya mitandao
‘Sijenibeba machela, pendaneni mpendao
Pepo za kisulisuli, zinavumisha mapenzi.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close