Ushairi

Nimewehuka.

NIMEWEHUKA
Uwanjani hana mwendo, anavyonipa uhondo
Mtoto mwanamitindo, nalisifu lake pendo
Kahitimu kwenye jando, kayahifadhi mafundo
Mahaba yameniteka, mwenzenu nimewehuka

Vile vyake vijimambo, hupenda kumwita chombo
Siyali tena makombo, kuichanganya mishombo
Avutia lake umbo, apendeza bila pambo
Mahaba yameniteka, mwenzenu nimewehuka

Yeye ndiye langu windo, mengine yabaki kando
Msumari mie nyundo, utamu wa muwa fundo
Ameninasa na tando, simuwezi kwa vishindo
Mahaba yameniteka, mwenzenu nimewehuka

Sitowafumbia fumbo, namsifia urembo
Hakukitumia chambo, mtego wake ulimbo
Wa kwangu fundi mitambo, naridhia majigambo
Mahaba yameniteka, mwenzenu nimewehuka

Chumbani mwangu midundo, uturi kote si vundo
Anavyocheza msondo, mwepesi kama kidondo
Chakula chake mandondo, mboga majani kibwando
Mahaba yameniteka, mwenzenu nimewehuka

Anayajuwa majambo, jina lake kwangu wimbo
Nimevishinda vigambo, rijali siendi kombo
Nimesahau kitambo, yalivyonitesa mambo
Mahaba yameniteka, mwenzenu nimewehuka

Namficha kwenye chondo, naridhia kwa vitendo
Hamadi kwenye kibindo, silaha yangu upendo
Wa malaika mwenendo, penzi nalipiga pondo
Mahaba yameniteka, mwenzenu nimewehuka.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close