Ushairi

Niishije.

NIISHIJE
Naja kwenu kwa heshima, salamu zipokeeni
Sitowapita daima, bila kuwapungieni
Nauliza kwa tadhima, mnijuze ihiwani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

Nawaomba nijuzeni, m’menishinda jamani
Nikitenda ihisani, mwanilipa nukusani
Wema hamuuthamini, chokochoko ni za nini
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

Nikikaanga omena, kapata mada jirani
Sasa nami nyama sina, wataka nipike nini
Hajanipa Subuhana, wanichunguzia nini
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Nikipata cha jioni, wauliza kala nini
Nikienda msalani, chooche ki rangi gani
Kwani wanitakiani, kujuwa ya kwangu ndani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Nikipika za majani, mchicha sukumawiki
Mboga zake ni majani, aliwapeza samaki
Yule hana na hanani, kwake nyumbani sifiki
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Yakwenu yamewashinda, ya kwangu mwayatakani
Vijiweni mwaniponda, sina kitu mfukoni
Wanafiki m’mewanda, umbea uso kifani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Maswali mwaulizana, yule ataoa lini
Amepita usichana, ataolewa na nani
Hata sura yeye hana, mwamkufuru Manani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi ?

Ukishika zako njia, ana maringo fulani
Huenda amefulia, kajifungia nyumbani
Pema ukiangukia, anaabudu shetwani
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

Kinalika shughulini, wajanicheka jirani
Kidhera ni cha zamani, ana majacha guuni
Kishati chake fulani, kilitoka mfukoni
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

Nawaaga kwaherini, nawaachia maswali
Mwenzenu niambieni, ‘sinyamaze kulihali
Menzamwenye ndo nyumbani, jina langu Danieli
Walimwengu nijuzeni, niishi nanyi kivipi?

(Daniel Wambua ndiye malenga wa shairi hili)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close