Ushairi

Nifunze mama.

NIFUNZE MAMA
Kwa jina la mola wangu, aloniumba Manani
Kanilinda wangu mungu, toka kwa mama tumboni
Ikafikia ya kwangu, kanileta duniani
Mama nifunze tabia, nisifunzwe na dunia

Kweli dunia ni chungu, ina mingi mitihani
Ni hadaa ulimwengu, ni wengi wa taabani
Siniache mama yangu, niwe kama hayawani
Mama nifunze tabia, nisifunzwe na dunia

Zimulike njia zangu, niendapo mitaani
Lisijeniteka wingu, la vibaka na wahuni
Wasizame ndugu zangu, kwa kuniiga mwendani
Mama nifunze tabia, nisifunzwe na dunia

Tumia hata kirungu, nikunje ningali chini
Nisiwe na wanguwangu, yanishinde uzeeni
Bora niwe chunguchungu, kwenye ndovu na kongoni
Mama nifunze tabia, nisifunzwe na dunia

Ninyoroshe mama yangu, niwe mja wa thamani
Uniepushe na pingu, za wabaya ikhiwani
Nikitegemee changu, nifupike mikononi
Mama nifunze tabia, nisifunzwe na dunia

Heshima yako mamangu, imbali na uduni
Nikuze kama wenzangu, na muongozo wa dini
Niiname cha mvungu, wakuu waniauni
Mama nifunze tabia, nisifunzwe na dunia

Dunia sio ya kwangu, nifunze kama mgeni
Nisijechemka wengu, nikazama machozini
Mama niite mwanangu, niitike pasi kani
Mama nifunze tabia, nisifunzwe na dunia.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Check Also

Close
Back to top button
Close
Close