Naomba suluhisho.
NAOMBA SULUHISHO
Mawazo jama mawazo, natambua chanzo chake
Huletwa na matatizo, kila mja ana yake
Mengine ni ya mizozo, furahayo yakupoke
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo
Mawazo huwa mazito, akili kuizuzua
Huleta kivangaito, lakufanya kutojua
Tumbo likawaka moto, na moyo ukaungua
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo
Hutia wengi vidonda, na kuchomeka moyoni
Kufanya wengi kukonda, waishie kaburini
Hasa yale ya kupenda, wengi wapo taabani
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo
Na mawazo ya maisha, ni wengi yamewatesa
Madhila yasiyoisha, yasopigika misasa
Kisha njaa huwatisha, tatizo hawana pesa
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo
Kuna yale ya kuatwa, matozi yabubujike
Na yakuumishe kitwa, mwendanio umzike
Mtima utaburutwa, ulie usononeke
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo
Mengine ni ya elimu, haswa kwa watahiniwa
Mitihani ni migumu, maishani wangojewa
Hutaki kujilaumu, cheti chako ukipewa
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo
Wengi sana hujiuwa, tamaa ikikatika
Sumu kule ikanywewa, uhai wakajipoka
Na vitanzi vikatiwa, mawazoni kupatoka
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo
Na mawazo huchakaza, na uso ukanyauka
Makunyanzi kuyajaza,surayo ikapauka
Huwezi kuyapuuza, mana moyo wachomeka
Natamani kulijuwa, suluhisho la mawazo.
(Malenga ni Daniel Wambua)