Ushairi

Nani angeweza.

NANI ANGEWEZA
Wanyama tuwafugao, hawa bata nao kuku
Watumie mbawa zao, wapuruke kule huku
Warudi mwituni kwao, wakaishi na kasuku
Hivi nani angeweza, kuwarudisha nyumbani?

Fahali wanaolima, wakatae katakata
Zikosekane na nyama, nani angewafuata
Waipange yao njama, kamba kuzikatakata
Hivi nani angeweza, kuwarudisha nyumbani?

Wanaokamwa maziwa, hawano warukeruke
Mori uwapande hawa, mazizini watoroke
Iwe ja wamepagawa, na mateke yatumike
Hivi nani angeweza, kuwarudisha nyumbani?

Na umbwa wawe wakali, wabweke kila mahali
Mbio ziso na mithili, wakimbie kulihali
Wapotee huko mbali, kunyamaze kuwe tuli
Hivi nani angeweza, kuwarudisha nyumbani?

Paka wasiwale panya, nyaunyau wende zao
Wasahau kuwa chanya, wakaishi na wenzao
Panya wapate mianya, ila nao wende kwao
Hivi nani angeweza, kuwarudisha nyumbani?

Na kondoo wageuke, mbio nyingi watimke
Manyoya yasisimke, hawa nao wakutoke
Kwa mikia teketeke, nyumbani wasioneke
Hivi nani angeweza, kuwarudisha nyumbani?

Punda nao watimke, wakawe pundamilia
Kwa milio waondoke, mizigo kuikimbia
Na rukwama ziachike, migongo kuirudia
Hivi nani angeweza, kuwarudisha nyumbani?

Ngamia wangalinuna, wema ukawatonoka
Wakauacha usena, upole ukawatoka
Wanyama wakaungana, majumbani kutoroka
Hivi nani angeweza, kuwarudisha nyumbani?

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close