Lugha na Sarufi

NAFASI YA KISWAHILI

NAFASI YA KISWAHILI KATIKA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI.UTANGULIZIKiswahili kimeibuka kuwa la muhimu katika tamaduni nyingi zilizopo Afrika Mashariki. Wakati wa enzi za ukoloni katika Afrika Mashariki,haja ya kuwepo kwa lugha moja itakayotumika hususan katika elimu katika nchi zote za makoloni ya mwingereza wakati ule,yaani Tanganyika,Kenya,Uganda ilijitokeza. Isitoshe, baada ya nchi nyingi za Afrika Mashariki kupata Uhuru, haja ya kuwepo kwa lugha moja kwa kila nchi kwa mawasiliano ilijitokeza waziwazi. Aidha kuwepo kwa makabila mbalimbali katika ukanda huu na maingiliano yazo katika shughuli mbalimbali kama vile biashara na nyinginezo za kijamii kulizusha haja ya kuwa na lugha moja ya kuunganisha. Hatua hizo zote zilichangia kwa Kiswahili kupewa hadhi na nafasi kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kama ifuatavyo.Lugha Kama Nyenzo Ya MawasilianoJukumu kuu la lugha yoyote ile ni kukidhi haya ya mawasiliano katika jamii yenye desturi moja.Katika ukanda wa Afrika Mashariki ,lugha ya kiswahili na ile ya kiingereza ndiyo hutumika. Lugha ya Kiswahili huweza kutumika katika maeneo ambamo kiingereza hakiwezi kutumika. Nchini Tanzania, Kiswahili hutumika kama lugha ya kitaifa, lugha rasmi katika shughuli za serikali na bunge, lugha ya mawasiliano katika shughuli za biashara za nchini na baina yake pamoja na nchi jirani. Nchini Kenya, Kiswahili hutumika kama chombo cha mawasiliano baina ya watu wa makabila mbalimbali, katika mikutano ya kisiasa na wananchi katika shughuli za biashara. Nchini Uganda, Kiswahili hutumika zaidi na askari na katika kufanya mawasiliano na wageni kutoka nchi jirani za Afrika Mashariki. Pamoja na kutofautiana katika viwango vya matumizi ya Kiswahili katika nchi za Afrika mashariki, bado linakuja swala la mawasiliano katika ngazi zote kwa watu wote, Kiswahili hupewa nafasi kubwa ukilinganishwa na nafasi inayopewa Kiingereza.Kiswahili pia kilitumika na polisi,sehemu za kaskazini pia na watu waliokuwa hawajui Kingereza na Luganda.Hivyo basi wanailotiki pia walitumia Kiswahili na makabila mengineLugha Ya Kiswahili Kama Kitambulisho Cha Jamii Ya Afrika MasharikiSwala la kuwa na kitambulisho cha watu wa Afrika Mashariki ilijitokeza baada ya viongozi wa ukanda huu kubaliana kuwaunganisha watu hawa ili lengo la maendeleo litimizwe. Njia ya kipekee ya kutambulisha hii lugha licha ya kuwa Kuna njia nyingine kama michezo,elimu,ushirikiano wa kiuchumi na hata kisiasa. Kwa sababu hii, lugha ya kiswahili ndiyo ingetumika kuwaunganisha watu wa Afrika Mashariki. Kupitia kwa hii, kiswahili kimeweza kuvuka mipaka ya nchi zao asilia yaani Tanzania na Kenya na kuenea kwenye nchi zote za Afrika mashariki. Kwa hivyo, lugha ya Kiswahili imepiga hatua kubwa kuwaunganisha watu wa Afrika mashariki kwa kuwa hamna lugha nyingine ya Kiafrika katika ukanda inayoweza kutekeleza jukumu hili. Kiswahili Kufundishwa Katika Shule Zilizoko Afrika MasharikiKiswahili kimetumiwa kama kiungo muhimu cha elimu kwa karibu nchi zote za Afrika mashariki. Pia kimetumiwa kufundishwa kutoka shule za msingi hadi chuo kikuu. Isitoshe, Kiswahili hutumika kutahini mitihani na hata kwa mazungumzo baina ya wanafunzi pamoja na walimu ili waweze kuelewana. Nchini Tanzania, Kiswahili ndiyo lugha ya kipekee inayotumiwa kufundisha katika nyanja zote za elimu kama vile shule ya msingi, sekondari na vyuo vikuu. Aidha, kiswahili pia ni somo la lazima kwa kila mwanafunzi. Nchini Kenya, Kiswahili hutumika pamoja na kiingereza kufundisha.Utungaji Wa Kamusi Za KiswahiliKazi za utungaji wa kamusi zimefanywa na wataalam wa lugha au asasi za lugha kama vile taasisi za Uchunguzi wa Kiswahili za taifa na kikanda pamoja na mabaraza ya Kiswahili ya taifa na kinda na hata watu binafsi kupitia lugha ya kiswahili. Kupitia hii, walimu na wataalam wameweza kuunganisha na lugha ya KiswahiliMatumizi Ya Lugha Ya Kiswahili Katika Vyombo Vya HabariKiswahili kimechangia pakubwa katika vyombo vya habari. Kwa mfano magazeti , redio na televisheni. Vyombo hivi vya habari vimesaidia kukisambaza kiswahili kwa haraka na kukuza uwezo wa lugha wa watumiaji wake. Kwa kuzingatia hali ya ushirikiano kampuni ya Nation Media Group ( NMG) ilibuni mradi wa kuendeleza jitihada za viongozi wa ukanda huu kwa kuunda mradi unaojulokana kama Swahili hub! Swahili hub ni mradi unaotumika kuweka pamoja kazi ya vyombo vya mawasiliano kama televisheni , redio na magazeti yaliyo chini ya NMG. Kuendeleza juhudi za kukiimarisha na kukiendeleza Kiswahili kwa wananchi wote wa nchi tano za jumuiya ya Afrika mashariki kama Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Tunayo pia wizara ya habari , michezo na utamaduni. Wajibu wake Ni kuwa na sera kwa kila fani inayosimamiwa ili kuona kuwa tuna taifa lenye maadili. Kupitia kwa hatua hizi, watu waweza kuunganisha pakubwa kwa kuwa vyombo hivi vya habari vimesaidia kukisambaza kiswahili, na watu wengi wamepata habari mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili.Aidha nchini Kenya Kiswahili kimetumiwa sana katika mitandao ya kijamii na blogu za watu binafsi. Vyombo vya habari vinavyotumia kiswahili nchini Kenya ni vingi na kinatumika katika programu kadhaa redioni na kwenye televisheni.Wataalamu wa Kiswahili,waandishi,wachapishaji,waimbaji na waigizaji wanayo fursa ya kutunga kazi zao na kupitisha katika magazeti ya mwananchi au mwanaspoti ambayo yanamilikiwa na kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) Kwa upande wa Tanzania na Taifa leo kwa upande wa Kenya. Kiswahili kama lugha ni nyenzo ya kuleta maendeleo katika sehemu mbalimbali za Afrika mashariki.
Uendelezaji wa kiswahili umeleta maendeleo katika sehemu mbalimbali za Afrika Mashariki kwani wanajamii hukitumia kuendeleza biashara zao, kufanya kazi mbalimbali hata kule mashambani, kufanya ukulima, kuuza bidhaa na shughuli nyingi za biashara. Biashara hizi hukuza uchumi wa wanajamii katika Afrika Mashariki hivyo huleta maendeleo.Kiswahili Hueneza Umoja Katika Jumuiya Ya Afrika MasharikiKiswahili kinaunganisha watu haswa kupitia ukalimani na utafsiri. Tafsiri katika maendeleo ya binadamu ni kubwa kutokana na ukweli kwamba tafsiri ndio daraja kati ya jamii mbalimbali za watu wanaotumia lugha zinazotofautiana. Hutumika kutolea maelezo , kwa mfano kwa biashara Kiswahili kitatumika kutafsiri bidhaa za watu, kiswahili kitatumika kueleza matakwa ya jamii fulani. Kwa hivyo kuleta umoja na amani.Kiswahili Hutumika Kueneza Hekima Na MaarifaKatika maeneo mengi yaliyomo Afrika mashariki, Kiswahili kinatumiwa kupitisha maarifa,hekima na pia maadili. Kwa baadhi ya shule, walimu hutumia lugha ya Kiswahili kuwafundisha wanafunzi maarifa. Pia kwenye ibada wahubiri hutumia lugha hii kueneza injili na maadili mbalimbali za kujikimu katika maisha.Kiswahili Hutumika Kukuza VipawaHukuza vipawa kwa vile Kuna wasanii wanaofanya kazi ya kuendeleza Kiswahili kupitia kwa sanaa. Wasanii hawa hutumia lugha ya Kiswahili kama kigezo cha kuunda nyimbo mbalimbali. Wanawakilisha na kuelezea watu kuhusu hizo nyimbo kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa hivyo wanajamii wenye uzoefu wa kusikiliza nyimbo hizo huwa wanaimarika kujua lugha ya Kiswahili. Vile wasanii hawa hukitumia Kiswahili kuwainua wengine wanaoanza usanii. Wanajamii pia wanatumia Kiswahili kukuza vipawa kama densi,uimbaji na vipawa vinginevyo katika Afrika Mashariki . Taasisi Ya Utafiti Wa Lugha Ya Kiswahili Ya Afrika MasharikiKuwepo kwa Kiswahili kumesababisha lengo la kuwa na asasi za kuendeleza Kiswahili. Wataalamu wamekuwa na haja ya kuwa na taasisi ya uchunguzi wa kiswahili ya kikanda. Taasisi hii imekuwa ya kitaaluma na pamoja na mambo mengine yanaweza kushughulikia miradi ya uendelezaji wa Kiswahili ya kikanda. Inaweza pia kuratibu semina, makongamano na mafunzo ya kikanda. Kwa mfano, mradi wa kamusi mama ya Kiswahili ambayo ameonyesha Kiswahili kama kinavyozungumzwa katika nchi mbalimbali za Afrika Mashariki inaweza kusimamiwa na taasisi hii.Matumizi ya Kiswahili Katika Bunge La Afrika Mashariki.Kiswahili kinatumiwa katika bunge la Afrika mashariki. Hi ni kwa sababu kiswahili kimefanywa kutumika katika nyanja zote na katika vyombo na asasi mbalimbali katika Afrika mashariki. Uamuzi huo sio tu utatoa changamoto kwa asasi nyingine bali pia utatoa ushawishi mkubwa kwa watu wa Afika Mashariki kukienzi,kukiendeleza na kukitumia Kiswahili katika maeneoUundaji Wa Ushirikiano Mpya Katika Jumuiya Ya Afrika MasharikiKatika miaka ya hivi karibuni, hususan baada ya kuanzishwa kwa sera za masoko huria, hali ya Afrika mashariki imebadilika sana. Hii inatokana na mwamko uliojitokeza miongoni mwa wananchi wa kawaida kujitokeza katika kufanya shughuli nyingi za biashara ambazo zamani zilikuwa zinafanywa na serikali au makampuni ya kitaifa au ya kigeni. Kwa sasa mchango wa watu wa kawaida Katika kuwafikia na kuwaunganisha watu wa Afrika mashariki ni kubwa mno ukilinganisha na ule wa serikali na makampuni ya kitaifa au ya kigeni. Wananchi wa kawaida ambao ni wafanyabiashara ndiyo kiungo kikubwa kwa sasa baina ya wazalishaji na wananchi. Maingiliano haya ambayo yatashika kasi jinsi ushirikiano mpya wa Afrika Mashariki utakavyokuwa unaendelea kukua na kutekeleza, yataanza kuibua suala la lugha ya kutumika katika kuwaunganisha na kuwashirikisha watu wengi zaidi na watu wa viwango tofauti vya elimu.Ushirikiano mpya wa Afrika Mashariki umefungua milango mingi ya ushirikiano katika nyanja za biashara,elimu,uchumi,kijamii na kisiasa. Iko azma ya kuwa na mipaka huru baina ya nchi husika, soko la pamoja la bidhaa za biashara baina ya nchi hizo, sarafu moja n.k.
Mazingira kama hayo yatafanya maingiliano baina ya watu wa Afrika Mashariki kuwa makubwa zaidi hususani kwenye nyanja za kiuchumi,kielimu na kijamii. Mazingira kama hayo yatanufaika zaidi kama Kiswahili kitatiliwa maanani katika nchi hizi. Hapa hatuna maana ya kusema kuwa kiingereza hakithaminiwi, bali tunachodai ni kuwa serikali zetu tatu zinatakiwa kuweka zaidi katika kupanua uelewa na matumizi ya Kiswahili katika kanda hii.Mwezi aprili, 2002, mjini Kampala Uganda kuanzia tarehe 8 – 11, kulifanyika kongamano la kikanda la nchi za maziwa making. Kongamano hilo ambalo liliandaliwa na mfuko wa mwalimu Nyerere , ilihusu uimarishaji wa mashirikiano ya kikanda na kuweka agenda ya milenia ya utamaduni wa amani, umoja na maendeleo ya watu. Katika kongamano hilo, pamoja na mambo mengine, suala la lugha lilipewa nafasi ya kuzungumzwa. Majadiliano kuhusu vyombo vya habari na maendeleo ya kiswahili yalibainisha mambo yafuatayo;
(i) Ukanda wa maziwa makuu unahitaji lugha ya kutambulisha na kuwaunganisha. Kiswahili ni lugha ambayo ilienea katika nchi zote za kanda hii na kwa hivyo iliaminika kuwa kinaweza kuzileta pamoja nchi zote katika kanda.
(ii) Kuendelea kutumia lugha za ulaya kama vile kiingereza na kifaransa kimechangia sana kukwamisha mawasiliano katika kiwango cha kitaifa na kikanda. Kiswahili kinaweza kutoa nafasi ya mawasiliano kati ya serikali na watu wake.
(iii) Kiswahili kimekwishaonekana kama lugha – mawasiliano iliyo bora na sio tu katika kanda ya maziwa makuu, bali pia katika Afrika.
(iv) Hadhi ya Kiswahili katika ukanda wa maziwa makuu hukifanya kiwe lugha pekee inayofaa kuendeleza kuwa lugha – mawasiliano ya kikanda. Ni lugha ya taifa katika nchi tatu katika kanda, inafundishwa shuleni karibuni katika nchi zote, na lugha ya mawasiliano miongoni mwa jamii za lugha mbalimbali za wenyeji.Maazimio ya kongamano kuhusu lugha ambayo yaliyosomwa mbele ya wakuu wa nchi za maziwa makuu, yaani Tanzania, Kenya , Uganda ,Rwanda ,na Burundi kabla hawajaanza mkutano wao wa kilele, yalisema kuwa kiswahili kinaweza kuchukua dhima ya kuwaunganisha watu katika kiwango cha kikanda. Hivyo, Kiswahili kipewe hadhi ya kuwa lugha – mawasiliano ( lingua franca) ya kikanda. Lugha nyingine zitakuwa na dhima zao katika kiwango cha kieneo kitaifa au kimataifa.Kiswahili kimechangia kuimarisha utamaduni . Kupitia kwa uchapishaji wa vitabu vya Kiswahili, tunapata kuelewa tamaduni za jamii tofautitofauti za wanajamii wa Afrika mashariki. Kwa mfano, kitabu cha utengano cha Said A. Mohammed kinaongelea utamaduni wa waswahili. Tunaweza hata kuona mambo yanayofanyiwa na wanajamii wengine kama mashindano ya nyimbo kwa kupitia lugha ya Kiswahili.HitimishoLugha ni chombo muhimu sana katika kuwaunganisha watu na kuwaleta pamoja . Hii ni kwasabababu jamii mbalimbali zina tamaduni tofauti ikiwemo lugha. Hii inajitokeza vema katika ukanda wa Afrika mashariki.
Ni kupitia tu katika kutumia lugha ya Kiswahili ndipo jamii hizi nyingi zitashirikiana na kuingiliana. Hivyo lugha ya Kiswahili ina nafasi kubwa katika kuleta mshikamano na ushirikiano baina ya jamii za watu wa Afrika Mashariki.MAREJELEOMulokozi,M.M.(2000). Language, Literature and the forging of a Pan African Identity Katika Kiswahili Journal, No. 63, uk. 71 -80.Nyerere foundation (2002).Brief for the leaders of the Region from the Symposium, Symposium on the Great Lakes RegionAsante, S.K.B. na Chanaiwa .D.( 1999).Upana Afrika na Ushirikiano wa Kikanda Katika Mazrui Ali A. na C. Wadji (Wahariri) (1999), Historia kuu ya Afrika, Juzaa iliyofupishwa, TUKI/ UNESCO: Dar es salaam.Whiteley, W. (1969). Swahili: ‘The Rise of a National Language. Methuen & Co LTD London.Massamba,D.P.B.(1990).Kiswahili kama Lugha ya Mawasiliano na Matumizi Yake Katika Vyombo Vya Habari.Makala yaliyotolewa katika Semina ya Kanda Kuhusu Sera na Mipango Ya Kushirikisha Vyombo Vya Habari Katika Kukuza na Kueneza Kiswahili Katika Nchi zinazotumia Kiswahili.

Tags
Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Check Also

Close
Back to top button
Close
Close