Ushairi

Mwenyezi Mungu Nakuomba.

***MWENYEZI MUNGU NAKUOMBA***
**
*
Rabbi naomba akili, nikutambue vilivyo /
Nisiishi kama zali, kufanya mambo ya ovyo /
Mizani isijefeli, motoni nifanywe chovyo /
Ya’Razzack Ya’Wadud, Allah nakuomba dua ////
*
Rabbi nomba amuali, itumike utakavyo /
Nifanye yalo jamili, nisitende yalo sivyo /
Dua yangu takabuli, upendalo liwe ndivyo /
Ya’Razzack Ya’Wadud, mjawo ninakuomba ////
*
Rabbi nomba ujalili, dunia akhera ndivyo /
Kwako hili ni sahili, thaura kwako ilivyo /
Mpanga yalo kamili, vyovyote vile iwavyo /
Ya’Razzack Ya’Wadud, mtumwawo ninaomba ////
*
Rabbi nomba umahili, kwenye vile nitendavyo /
Niepushie batili, niwe halali kiivyo /
Siku ‘kikata kauli, pengo langu lonekavyo /
Ya’Razzack Ya’Wadud, goti kwako nimepiga ////
*
Rabbi naomba husnuli, khatma vyovyote iwavyo /
Jannat nikavinjali, na vile vitu vilivyo /
Usinifanye anzali, nikawa wa ovyoovyo /
Ya’Razzack Ya’Wadud, Mola wangu msikivu ////
*
Sita beti za usuli, uchache dua ilivyo /
Kama ndanimwe ulili, Mwenyezi ufanye ndivyo /
Mie kiumbe dhalili, ninaomba niwazavyo /
Ya’Razzack Ya’Wadud, mpanga usiye shaka ////

(Malenga ni Bin Omary)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close