Ushairi

Mshairi si mwenzio sindane naye.

MSHAIRI SI MWENZIO
HUWEZI SHINDANA NAE

Anashinda akitunga
Atengeneza mizani
Vina anavyovipanga
Vyote vitoke kichwani
Na sio kuungaunga
Hiyo ndio yake fani
Mshairi si mwenzio
Huwezi shindana nae

Tungo anazozifunga
Za kisasa na zamani
Paka kuitwa malenga
Ni msoto si utani
Na sio kuzibananga
Ajua afanya nini
Mshairi si mwenzio
Huwezi shindana nae

Mashairi yanakonga
Yapita paka moyoni
Beti akizikaanga
Kuzisoma tatamani
Leo wewe unachonga
Ushairi kazi gani
Mshairi si mwenzio
Huwezi shindana nae…

Atunga kuwapa mwanga
Kwa waliopo gizani
Huyatungia majanga
Yaliopo duniani
na hutunga zake kunga
Vizuri kwa umakini
Mshairi si mwenzio
huwezi shindana nae

Akitaka kukunanga
Hukunanga kwa mizani
Na hujitoa muhanga
Kupinga jambo fulani
Hawezi kuwa mjinga
Ni kubwa yake thamani
Mshairi si mwenzio
Huwezi shindana nae

Washairi ni wahenga
Wapogo toka zamani
Tungo zao zililenga
Na zenye mafunzo ndani
Walikaa wakalonga
Kuikuza hii fani
Mshairi si mwenzio
Huwezi shindana nae

Nakipuliza kipenga
Nimeshafika mwishoni
Sijaja kuwasimanga
msio na hii fani
Na sisemi tunaringa
Ukweli naubaini
Mshairi si mwenzio
Huwezi shindana nae.

(Mtunzi:Bintrasool)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close