Ushairi

Miluzi.

Mwaambaje waambaji, wenye ndimi za wahenga
Mambo kwangu ni saruji, sina tiba wala kinga
Nipo kama mfa maji, kushika hata mchanga
Nawapigia miluzi, niwajuze nipo hai

Hata japo nimekonda ,na ngozi imesinyaa
Naamini nitashinda, familia kuifaa
Wale wanaoniponda, wabaki wakibung’aa
Nawapigia miluzi, niwajuze nipo hai

Viganja vimechubuka, nikifanya za sulubu
Mijasho kububujika, usiku ndimi bawabu
Miundi imefyonzeka, ulaji ndio sababu
Nawapigia miluzi, niwajuze nipo hai

Binadamu nao ngamba, kelele nazisikia
Kutwa kucha wanatamba, matusi nayasikia
Wale warabu wa pemba, wasema nimefulia
Nawapigia miluzi, niwajuze nipo hai

Hakika misukosuko, ndo iliyonipoteza
Ilitoboka mifuko, nikawaza lakuwaza
Vilipozidi vituko, mwenzenu nikanyamaza
Nawapigia miluzi, niwajuze nipo hai

Upepo waniyumbisha, kama bua la mahindi
Dunia yanifundisha, kusikoendwa siendi
Jua linaniyeyusha, fani tena haipandi
Nawapigia miluzi, niwajuze nipo hai

Natumai nitarudi, nitarudia utunzi
Nitakuja na juhudi, kama mruka vihunzi
Kama ua la waridi, nitaliwaza wapenzi
Nawapigia miluzi, niwajuze nipo hai.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Check Also

Close
Back to top button
Close
Close