Mbona nisirudi.
Natamani nikarudi, siku zile zamani
Ila tu imenibidi, uwezo sina sinani
Nami ningejitahidi, pale ninapotamani
Ila sasa nifanyeje, jua litarudi nyuma?
#
Natamani zama zile, zisokuwa na potole
Lipopiga ukelele, nihudumiwe wavyele
Ya kesho nisiyaole, vya shubiri nisivile
Ila sasa nifanyeje, jua litarudi nyuma?
#
Mambo ya kukosa kazi, katu nisiyaelewe
Kodi ikawe upuzi, nisikie kwa wenyewe
Sinao hata mchuzi, nyumba nje kafungiwe
Ila sasa nifanyeje, jua litarudi nyuma?
#
Lakini ningejipanga, kuyafanya maamuzi
Singekuwa tena bunga, nikashinde kwa upuzi
Kuovu singejiunga, ningeenda na wajuzi
Ila sasa nifanyeje, jua litarudi nyuma?
#
Ningeepuka ushenzi, na kuwinga kwa ukali
Nikijua hilo penzi, kamwe haliwi ugali
Kwangu ngekuwa mlinzi, nikaishi kisahili
Ila sasa nifanyeje, jua litarudi nyuma?
#
(Mlumbi Mtafumaniwa Okelo)