Ushairi

Mashairi yanayozuzua.

TUACHE MATAMANIKO.

Karibuni nisongele, kaeni kwa mzunguko,
Kigodani niketile, nitemele mzinduko,
Wenye mvi linemele, tamaa ni maanguko,
Tuache matamaniko, mauti situfikile.

Umero jipu tumbule, huyaleta masumbuko,
Utake hili na lile, hadi kufanya tambiko,
Huoni wang’oka nywele, na hupati tuliziko?
Tuache matamaniko, mauti situfikile.

Kiwa mepata mawele, kubali ndiyo ya kwako,
Mbona utake mchele, na sio kiwango chako?
Rahimu nd’o mgawile, siletile chokochoko,
Tuache matamaniko, mauti situfikile.

Ukipata kitungule, shukuru kwa goti lako,
Siwe mpiga kelele, wa kumtaka kiboko,
Watakani kubwa wele, ya dunia mapitiko?
Tuache matamaniko, mauti situfikile.

Tamaa ikiwa mbele, nyumaye huwa mauko,
Tulambiwa enzi zile, kwa lugha msisimko,
Toka tuigeukile, twaranda ja mbwakoko,
Tuache matamaniko, mauti situfikile.

Uroho sikutawale, lichonacho ndicho chako,
Cha mwenzi sitamanile, kakupata fadhaiko,
Vitakumea vipele, vikupeleke maziko,
Tuache matamaniko, mauti situfikile.

Tamati napakomele, sitaki vyenu vituko,
Mtima niufungule, wazi bila mafumbiko,
Mwoshashombo ndimi yule, noshaye mtakatiko,
Tuache matamaniko, mauti situfikile.

(Allan Lumunyasi Chevukwavi Mwoshashombo).

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close