Ushairi

Mashairi ya Kiswahili.

………… MWALIMU NAANGAMIA ……….
mwalimu ninalilia, machozi yatiririka
Serikali saidia, mwalimu ninateseka
Nani atanikwamua, majanga yameniteka
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Mbona ninasahaulika, mwelekezi wa shuleni
Bunge sijatambulika, wakiwepo kikaoni
Wabunge mnanizika, ninaenda kaburini
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Tufanyapo mtihani, mwalimu ninasifika
Nizamapo taabuni, jamii inanizika
Niende wapi jamani, nchi imenigeuka
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Mwajiri niliamini, sasa amenigeuka
Ninakoishi nyumbani, mwenyewe akasirika
Nilikokopa dukani, kooni amenifika
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Enyi nilowachagua, njooni mniauni
Kura niliwapigia, mnitoe taabuni
Nyote mmenipotea, sijawaona machoni
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Kenyatta nilichagua, kwenye seneti Malala
Tindi nilimpigia, tangu aliposimama
Siaya ninatokea, Rasanga niliungama
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Nawalilia wazazi, ninaowafundishia
Nimesema tangu juzi, ombi kunisaidia
Sina pato wala kazi, nyinyi nawategemea
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Maulana nijalie, na cha kutia tumboni
Nani nikamlilie, kama si wewe Manani
Sin’ache niangamie, nilivyofanywa nchini
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Walokuwa marafiki, kitambo walinitenga
Nimebaki kwenye dhiki, Rabana ananichunga
Kubembeleza sichoki, kwa maombi nitafunga
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo

Kwa kweli sina hakika, nitarejea shuleni
Huenda yakanifika, yanitue kaburini
Iwapo yatatumika, nchi yangu buriani
Mwalimu naangamia, sina kazi wala mlo
WALIMU IPO SIKU. KILA MARA WANATUTIA MOYO KUWA NI MUNGU AWEZAYE KUTULIPA. HATIMAYE KAULI HII IMETIMIA. HATUNA WA KUTULIPA DUNIANI. TUNATARAJIA SAA YA MUNGU. Mwalimu Sammy nimelitunga shairi hili si kujisifu kwa vikombe nilivyoshindia shule mbalimbali, si kusifia utunzi wangu wa mashairi bali kuwasilisha vilio vyetu kwa amina. IPO SIKU.
#SavePrivateandBOMTeachers
CC Citizen TV Kenya
#StateHouseKenya
#NTV
KUTV – Mawimbi ya Lugha

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close