Ushairi

Mashairi Murua ya Kiswahili.

KOSA LA KWANGU NI LIPI?

Ukowapi Maulana, kiumbe chako nadai,
Ili tuweze kunena, yapo kwangu hayafai,
Ni wapi tulitengana, waziwazi nakurai,
Kosa la kwangu ni lipi, kwa nini sifanikiwi?

Tangu kule utotoni, nilivyofika dunia,
Hadi sasa ukubwani, maishani najutia,
Jitihada za shuleni, ni wapi zimehamia,
Kosa la kwangu ni lipi, kwa nini sifanikiwi?

Ibada sijasusia, naenda kila wakati,
Ninaamini ni njia, kukuambia ya dhati,
Zaka na sadaka pia, hapo sijakusaliti,
Kosa la kwangu ni lipi, kwa nini sifanikiwi?

Hata na changu kipawa, cha kuandika shairi,
Nimetumia nikiwa, chuoni na sekondari,
Ila sijafanikiwa, yanaibwa na hodari,
Kosa la kwangu ni lipi, kwa nini sifanikiwi?

Meandika vibarua, ili kusaka ajira,
Naambiwa nasumbua, hadi naitwa fukara,
Wengine wazichukua, wazirarua kwa sura,
Kosa la kwangu ni lipi, kwa nini sifanikiwi?

Mashimo nimeyachimba, hata kazi za sulubu,
Hata na kule kwa shamba, bado pia pana tabu,
Nikilima ninavimba, yananifwata sarubu,
Kosa la kwangu ni lipi, kwa nini sifanikiwi?

Waliozaliwa jana, hasa nilotangulia,
Wanaishi vyema sana, hakika wanavutia,
Hakuna kitu hawana, au cha kung’ang’ania,
Kosa la kwangu ni lipi, kwa nini sifanikiwi?

Maulana nipe yangu, nimechoka kumezea,
Kumezea ndugu zangu, huku wakinizomea,
Wemenizomea tangu, siwimi nalealea,
Kosa la kwangu ni lipi, kwa nini sifanikiwi?

(Toney Francis Ondelo-Malenga Mjalisiha)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close