Ushairi

Mashairi bora ya Kiswahili.

Nisifu nikiwa hai, Nisikie nifurahi
Usingoje nizirai, ama kifo kiniwai
Sifa zako anuwai, Nikifa hazinifahi
Nizike ningali hai.

Unisifu nikinai, kwa furaha nijidai
Kuongeza ni jinai, Sema kweli si madai
Sitazua vurumai, bora uwe huadai
Nizike ningali hai.

Msaada sikatai, Sizioni zenu chai
Kwa taabu sijifai, mko kimya ngali hai
Kaburini kirishai, michangoni mwajidai
Nizike ningali hai.

Suti Kali yenye tai, Mwanivisha na si hai
Mara pilau kwa yai, Munakula walaghai
Sifa zenu sizivai, Sijimanyi mi ‘Mgai’
Nizike ningali hai.

Wala hamujishangai, Mlikuwa hamufai
Leo sinao uhai, Kunijali mwajidai
Sifa zenu hazijai, Kaburini hazikai
Nizike ningali ngai.

Tafadhali nawarai, Nifaeni ngali hai
Kama Ng’ombe na Masai, Nifaeni nifurahi
Niwapapo baibai, Sifa zenu nisabahi
Nizike ningali hai.

(Mtunzi:Duncan Mulu)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close