Ushairi

Mapenzi.

Siendekezi mapenzi, yakanitia wazimu
Siku hizi ni ya tenzi, hayana tena nidhamu
Unayemwita mpenzi, anachepuka kwa zamu
Kama wewe nawe ng’ombe, ukamuliwe na nani?

Waloyafanya buhumu, walipoteza uhai
Yamekuwa ya misimu, bila noti haufai
Kutele wanaharamu, wa ndoa wana nishai
Kama wewe nawe ng’ombe, ukamuliwe na nani?

Marijali wanafuka, mabanati wanawaka
Mahaba yamebisika, bila mali waachika
Warembo walorembeka, mwenzako kagharimika
Kama wewe nawe ng’ombe, ukamuliwe na nani?

Cha mtenda na mtendwa, mtumwa na mtumiwa
Mpondwa naye mpendwa, waume wadhulumiwa
Mababe walishashindwa, seuze ewe mkiwa
Kama wewe nawe ng’ombe, ukamuliwe na nani?

Vitanzi na fumanizi, vidonda tele moyoni
Bora uitwe mpuzi, kwa kuwazuga ugani
Ukijuwa huna kazi, kwenye viti kaa chini
Kama wewe nawe ng’ombe, ukamuliwe na nani?

Wamhonga akahonge, wanunua akapewe
Yako yaende mvange, mwenzio atonokewe
Mapenzi yana mawenge, bora hadithi za mwewe
Kama wewe nawe ng’ombe, ukamuliwe na nani?

Natamani nisipende, moyo ususe kabisa
Nichukiwe chondechonde, kama mvua iso pusa
Siwataki walimbwende, kutwa kucha na misasa
Kama wewe nawe ng’ombe, ukamuliwe na nani?

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close