Mapenzi yamejaa upungufu.

Mapenzi sio kipofu, yana mato siku hizi
Yanachagua minofu, hayavutwi kwa hirizi
Yamejivisha jokofu, la usaliti na wizi
Yamejaa upungufu, hayana tena mjuzi
Mapenzi bila sarafu, kama wali uso nazi
Itakuingia hofu, umegewe waziwazi
Upewe hadithi ndefu, uambe ni kikohozi
Yamejaa upungufu, hayana tena mjuzi
Mababe leo magofu, hawaimbi ni miluzi
Wamekuwa kama wafu, si wa leo si wa juzi
Wamevaa nguo chafu, sera katu hawauzi
Yamejaa upungufu, hayana tena mjuzi
Walibwagwa chini tifu, walioyapiga mbizi
Wakapata maumbufu, kuyafua kumbe nazi
Wakatamani barafu, wayapoze mauguzi
Yamejaa upungufu, hayana tena mjuzi
Wasemao wazoefu, wale wenye mazoezi
Walichomeka mapafu, magumu wakamaizi
Walishindwa kuwakifu, wale wao wapumbazi
Yamejaa upungufu, hayana tena mjuzi
Huwavutia harufu, wakazitafuta ngazi
Ila wakijayashufu, yamejaa mazigazi
Wangavaliwa mikufu, bora wawe wafagizi
Yamejaa upungufu, hayana tena mjuzi
Walokuwa wakunjufu, walitolewa machozi
Wakaacha kuyasifu, akina mandanda kozi
Wakarudi kwa Raufu, wakajuwa hawawezi
Yamejaa upungufu, hayana tena mjuzi
Kamwe sitoyakashifu, wapendana hata mbuzi
Nayaweka kwenye safu, vijiandae vizazi
Hakuna uaminifu, yalobaki utelezi
Yamejaa upungufu, hayana tena mjuzi.
(Malenga ni Daniel Wambua)