Ushairi

MALIMWENGU

Shairi la maliwengu

MALIMWENGU

Jamani jama wandani, moyoni ninaumia,

Naloa damu kwa ndani, lazma mle tagandia,

Hata huku wajihini, kunyanzi yanivamia,

Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Najiita hayawani, kwa udhia wa dunia,

Masumbuko manyumbani, uzee unaingia,

Matusi ya hadharani, matumbo yanaumia,

Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Hata ninapojaribu, mathalani kuridhia,

Hayupo wa kunitibu, kukichapo ninalia,

Majanga yananisibu, wapi n’takimbilia,

Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Nimejaribu jirani, yote haya kumwambia,

Kumbe sivyo nivyodhani, jirani anazamia,

Ashaikula yamini, rohoye kujikatia,

Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Hata nao marafiki, mijini wamehamia,

Wote walioashiki, siwezi kuwafikia,

Wengineo mafasiki, maisha wanojutia,

Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Nilijaribu kusoma, kazi kuikimbilia,

Vitabuni nilizama, aushi kupigania,

Haya yanoniandama, sikujua tapitia,

Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

Rahimu mwenye huruma, jikaze hima Jalia,

Mpaji wa yalomema, nipe nije furahia,

Vicheko vije kukoma, nami nije shangilia,

Nitajifichia wapi, malimwengu menichosha.

(Malenga ni Toney Francis Ondelo)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close