Ushairi

Malenga nakulilia.

MALENGA NAKULILIA
Zile tungo zangu Dani, kumbe hazijatimia
Kule kwao makundini, mwenzenu sijafikia
Sitokata tumaini, Mola atanijalia
Jalali Mola Karima, malenga nakulilia

Niliwakanyaga nyoka, wote wakanirukia
Pangoni wakakutoka, nasaha kunipatia
Mawazo yakanitoka, fani nisijekimbia
Jalali Mola Karima, malenga nakulilia

Nilijuza ta Nassiri, ‘malenga naukimbia
Akanipa ushauri, wala nisijejutia
Ni ndefu hino safari, yahitaji vumilia
Jalali Mola Karima, malenga nakulilia

Nionyeshe nami ndia, niate kulialia
Nijalie mi radhia, ndoto zangu kutimia
Nyatunyatu nanyatia, kileleni kufikia
Jalali Mola Karima,malenga nakulilia

Weledi wakiridhia, tungo zangu tatulia
Tena nitajivunia, hongera kujipatia
Wengi nitawaambia, ni moyo na Mola pia
Jalali Mola Karima, malenga nakulilia

Diwani nitachapisha, jina kujitangazia
Na nitawahamasisha, wale wanotamania
Wala sitojifurisha, kifua kujipigia
Jalali Mola Karima, malenga nakulilia

Nitawakumbuka sana, jeki walonipigia
Ni wengi tena sana, Mola atawajalia
Siku nikijulikana, nanyi nitawafikia
Jalali Mola Karima, malenga nakulilia

Kama Mola ndo mpaji, ya kwangu itafikia
Tena atanifariji, vizuri kunipatia
Sijifanyi mjuaji, makaa kujipalia
Jalali Mola Karima, malenga nakulilia.

(Daniel Wambua-Malenga)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close