Ushairi

Majani

MAJANI
Majani yapukutika, makavu hata machanga
Wanyama wasononeka, wayamaliza mchanga
Machozi yanawatoka, ni hatari hili janga
Mbona yaanguke vino, na mvua yanyesha mno?

Rangi ya chanikiwiti, imekolea mitini
Miche yenye baidhati, yanyofolewa majani
Majani yalo huluti, yamezua tafarani
Mbona yaanguke vino, na mvua yanyesha mno?

Hali haiko shuari, rangi nzuri yapotea
Turudini kwa kahari, majani yatokomea
Hata japo si dahari, yaumu tuongezea
Mbona yaanguke vino, na mvua yanyesha mno?

Wanyama watoka mbavu, kwa njaa pia kulia
Kungalikuwa kukavu, kwingine wangehamia
Yangalikuwa mabovu, wao wangavumilia
Mbona yaanguke vino, na mvua yanyesha mno?

Lau yangatobolewa, wadudu kuyavamia
Rangi ya njano kupawa, kwetu yangatufikia
Vinywa tusingepanuwa, moyoni yangasalia
Mbona yaanguke vino, na mvua yanyesha mno?

Kila kunapo kuchele, habari zingaenea
Wanyama wote kelele, majani yapomokea
Halijawa na uwele, mtini lingapotea
Mbona yaanguke vino, na mvua yanyesha mno?

Majani yaso na nyaka, chini yanatangulia
Yale yalo na viraka, nayayo yafuatia
Wanaatiwa kumaka, wanyama walotulia
Mbona yaanguke vino, na mvua yanyesha mno?

Namuomba Rahamani, majanga kutu’ndoleya
Tuishini kwa amani, siku zetu kufikiya
Nimefika kikomoni, malenga nawakimbiya
Mbona yaanguke vino, na mvua yanyesha mno?

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Check Also

Close
Back to top button
Close
Close