Ushairi

Kumbuka mwanadamu.

KUMBUKA MWANADAMU
Hakika ya mwanadamu, utambaye ardhini
Ulosahau Rahimu, wajitapa duniani
Rabana humheshimu, wajigamba kwa mapeni
Miliki hata bahari, makaziyo mwanandani

Kusali huna wakati, Mola wako humtaki
Shetwani kakuthibiti, kwake gizani hutoki
Umebebwa hatihati, mwanadamu huzinduki
Uliumbwa mwanadamu, umsujudie Allah

Umejawa na kiburi, hukumbuki jehanamu
Waabudu utajiri, pesa kwako ndo muhimu
Wamkufuru Kahari, kiama hukifahamu
Ewe mja nakusihi, mtubie Mola wako

Ujana umekuteka, ardhini una ndweo
Anasa ziso mipaka, midundo ya mamboleo
Wapata unachotaka, ila huna mwelekeo
Kuna kifo mwanadamu, na hutoishi dahari

Mbona tusijiandae, kwa maisha ya keshoni
Anasa tuzikatae, tukapenyezwe peponi
Umepata upendae, wasahau kaburini
Tuishipo duniani, tukumbuke kaburini

Rohoyo itolewapo, uchungu uso kifani
Uwapendao hawapo, na hawatakuauni
Muda wako ufikapo, ukatiwe kaburini
Adhabu ya mle ndani, mwenzangu hutoiweza

Kuna nyoka anauma, mfano wake hakuna
Kila swala ‘takuuma, si usiku si mchana
Giza litakuandama, usaidizi hakuna
Adhabu hino jamani, kuiepuka ni swala

Kuna rungu kubwa sana, malaika wasubiri
Dhambi zako ewe mwana, azinakili Nakiri
Hutoikumbuka jana, ujibupo Munikari
Maswali haya wenzangu, ni mazito tena sana

Hivi nani Mola wako, utashindwa kulijibu
Na ni ipi dini yako, utamani uwe bubu
Subiri hukumu yako, litakuliza muhibu
Hino dunia si yetu, tujiandae ahera.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close