Kinanuka.

KINANUKA
Uzuri wa mkakasi, ndani kipande cha mti
Ningalikuwa jasusi, ningatoa ithibati
Chengoni kama msasi, nimefanya utafiti
Ukikinusa makini, kinanuka fondogoo
Hata kingameremeta, metu mithili dhahabu
Mwendo kingajiburuta, kuvutia maswahibu
Gizani kwenye usita, kingalilizua gubu
Ukikinusa makini, kinanuka fondogoo
Gubigubi kingatanda, kikakolea nidhamu
Kikavishwa pete chanda, wengi wakakifahamu
Ila ndani ni vidonda, vilojaa tele sumu
Ukikinusa makini, kinanuka fondogoo
Kama usiku wa kiza, hutoziona kasoro
Mgeni ungakituza, kama sanamu mchoro
Tena kingakuliwaza, kwa vinyimbo vya upyoro
Ukikinusa makini, kinanuka fondogoo
Kule kwao pekupeku, hakina utu kahini
Maneno kama chiriku, nzi wafia dondani
Kesho ukiwa kapuku, chageuka mhaini
Ukikinusa makini, kinanuka fondogoo
Kipya kinyemi hakika, ila vingi ndivyo ghushi
Leo kesho kinawaka, mtondo chawa kizushi
Manzilini chalipuka, na zahama vifurushi
Ukikinusa makini, kinanuka fondogoo
Kinganukia uturi, kikutie mtegoni
Kikunase kwa ghururi, ja matumbo na maini
Ujihisi halibari, kikufunike machoni
Ukikinusa makini, kinanuka fondogoo
Mapema nakishonoa, nta nanyi mzitoe
Sote tungakidondoa, malengo kisibomoe
Nawasihi chadokoa, chonde kisitutoboe
Ukikinusa makini, kinanuka fondogoo
(Malenga ni Daniel Wambua)