Ushairi

Kila la heri mwereni.

KILA LA HERI MWERENI
Salamu zangu nawapa, kaka yenu muadhamu
Niwambie pasi pupa, jambo lililo muhimu
Mtihani si mfupa, kwenu usiwe mgumu
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Muda sasa umefika, wa kuyavuna mapando
Kwa walimu sina shaka, waliwalisha uhondo
Mwisho atakaye cheka, hucheka kwacho kishindo
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Alopanda pametosha, mwambieni aamke
Atavuna pamekwisha, jina la shule lishuke
Walimu wakifundisha, kaeni ange mshike
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Ng’ombe msham’maliza, mkia usiwashinde
Mwishoni mkateleza, nawasihi chondechonde
Kamwe msije kucheza, Malaika wawashinde
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Katu msitetereke, bidii kuipunguza
Muda bado msichoke, mkajawa mapuuza
Nawaomba mdamke, vitabu kuvitukuza
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Someni kana ya kwamba, kesho hamsoni tena
Vilo chini kuvichimba, akilini kuvishona
Ngurumeni kama simba, wenye njaa zilo nona
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Kuweni sana karibu, huno muda na walimu
Maswali yakiwaswibu, kuwaona ni muhimu
Dokita watawatibu, keshoni mtahitimu
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Usiwapenye uzembe, mkaanza kujisifu
Kwa mola sana muombe, awalindeni Raufu
Siku chache msiyumbe, shikeni njia nyoofu
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Hadhi ya shule kudumu, ni nyie washika dau
Jaeni nyingi hamumu, wajawazito falau
Nawaachia hatamu, ishikeni angalau
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

Izidisheni nidhamu, kwa walimu wenu pia
Katu wasiwalaumu, nukusi kuwatilia
Naiangusha kalamu, hapa kumi nakwamia
Mwereni kila la heri, nawaombea Wambua

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close