Ushairi
Jitokeze nikuone.

JITOKEZE NIKUONE
Yuko wapi nauliza, mwenye mapenzi ya dhati?
Kipusa wa kupendeza, mtego kwa ‘tanashati?
Asiyependa kuliza, na akipenda hasiti?
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.
Aliye na umbo nzuri, aibuaye hisia?
Mtamu kama sukari, ‘kimbusu najifia?
Nihisi mie ushwari, na akinikisi pia?
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.
Fundi wa kusasambua, tena bila kusumbua?
Na kiuno kunengua, tena bila kutegua?
Katu sitomzingua, ‘tampenda atambue,
Kipusa pale ulipo, jitokeze n’kuone.
(MTUNZI:Kongowea)