Ushairi

Jicho punguza upeo.

Kuona ni kazi yako , ila sasa waniponza
Vitu vikipita kwako , moyoni vyaniumiza
Punguza makali yako , vyengine wewe puuza
Jicho punguza upeo , moyo uweze tulia

Japo hauna pazia , mlango wako we funga
Watu wakikubishia , tena jaribu kuringa
Tena wakikuchachia , wapuuze na kusonga
Jicho punguza upeo , moyo uweze tulia

Watesa sana ulimi , kusema usoyataka
Ukiona kijimami , ulimi unakisuka
Ila ukigonga lami , moyo una taabika
Jicho punguza upeo , moyo uweze tulia

Unaitesa akili , huko kwako kupepesa
Mengine ya idhilali , ambayo moyo hugusa
Na wajiona fahali , jicho acha kunitesa
Jicho punguza upeo , moyo uweze tulia

Si vyote vinovutia , ladha yake huwa nzuri
We baki kuangalia , usitamani safari
Mana vikikufikia , hutoimudu bahari
Jicho punguza upeo , moyo uweze tulia

(MTUNZI:HANAFI MWINYIATANI)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close