Ushairi

Jamvi nimelinunua.

Nasema na walimwengu, wasiopenda kuona.
Kwa sasa mie ni changu, lakini mnashindana.
Heshima kwanza wenzangu, tusije kufarakana.
JAMVI NIMELINUNUA, TAMAA YENU YA NINI?

Mate kwenu yawatoka, kila mnapo liona.
Hongera mwanipa kaka, jamvi langu limefana.
Kumbe ndo mnalitaka, kukaa mnashindana.
JAMVI NIMELINUNUA, TAMAA YENU YA NINI?

Kama ni kweli wataka, nawe nunua la kwako.
Mwenzenu nayatamka, msikiweke kitako.
Jamvi langu nalitaka, toweni na mhemeko.
JAMVI NIMELINUNUA, TAMAA YENU YA NINI?

Nilituma wangu jomba, pesa kuninunulia.
Ni bora tuwe mwanyumba, dadake amebakia.
Sitaki ndoa kuyumba, hilo jamani sikia.
JAMVI NIMELINUNUA, TAMAA YENU YA NINI?

Undugu tutavunja, usipochunga jirani.
Jamvi langu nitakunja,litabakia nyumbani.
Atanipakia wanja, nitazamapo machoni.
JAMVI NIMELINUNUA, TAMAA YENU YA NINI?

Ni mbali niliko kwenda, kutafuta langu jamvi.
Tena mnipe kidonda, sija ziota na mvi.
Hasira zitanipanda, sababu ni langu jamvi.
JAMVI NIMELINUNUA, TAMAA YENU YA NINI?

Habari mumeipata, ninakatisha kauli.
Na nena huku nasita, kwa kweli sinayo hali.
Chunga nisije kukuta, nitakupeleka mbali.
JAMVI NIMELINUNUA, TAMAA YENU YA NINI?

(MTUNZI:SAID MRUU)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close