Ushairi

Huwezi.

HUWEZI
Unavyoamini sivyo, mwanamwali wajitesa
Huwezi nibeba ovyo, mie kwako nilisusa
Ungafahamu yalivyo, mvua yako ingapusa
Wameshindwa wenye pembe, kipara hutoniweza

Tipwatipwa walishindwa, kimbaumbau huwezi
Jino wala si kupendwa, nikuonyeshwa ufizi
Kimapenzi hujafundwa, leo nakuweka wazi
Wameshindwa wenye pembe, kipara hutoniweza

Maringo yaso kiini, kwangu mimi siyajali
Ukiwa hurulaini, kukupenda ni muhali
Katu sitokutamani, bora nikatendwe mbali
Wameshindwa wenye pembe, kipara hutoniweza

Mwanzoni nilikupenda, ukataka iwe siri
Kumbe kule waniponda, najichezesha kamari
Rijali yakanishinda, madhilayo furifuri
Wameshindwa wenye pembe, kipara hutoniweza

Kule kwangu kukusihi, ubadili yako ndia
Kamwe hukutanabahi, kejeli kunifanyia
Kumbe yupo kaniwahi, ukashindwa kunambia
Wameshindwa wenye pembe, kipara hutoniweza

Nakuchamba hadharani, hili mie sikufichi
Siwezi enda dukani, kisa heti niko uchi
Nguo zitele nyumbani, siwezi tembea uchi
Wameshindwa wenye pembe, kipara hutoniweza

Vimejazana vionzi, vya kijani kwenye simu
Jumbe nyingi za mapenzi, yani kama mhudumu
Nawaliwaza kwa tenzi, penzi nawapa kwa zamu
Ja kozi mwanamandanda, kulala njaa kupenda.

(Malenga ni Daniel Wambua)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close