Hadi connection.

Chuo nimeshahitimu, koneksheni ajira / Kitaa mambo magumu, huonekani ujira / Nazidi kosa stimu, kama tumbo la kuhara / Maisha bila “konekti”, katu huwa hayaendi ////
* Nataka kwenda peponi, “koneksheni” nijuzwe / Asbabu nibaini, ‘badani nisipotezwe / Na nifishwe kiumini, nnari nisiingizwe / Maisha bila “konekti”, katu huwa hayaendi ////
* Mchumba nimekupata, “koneksheni” walii / Vipi kwenu nitapeta, niiongeze bidii / Kile watachokipata, wanione ni mtii / Maisha bila “konekti”, katu huwa hayaendi ////
* Ukapuku menikifu, “koneksheni” ‘tajiri / Iwapi mniarifu, nami nitafanya siri / Isimuudhi Raufu, kwa kufanya ya sihiri / Maisha bila “konekti”, katu huwa hayaendi ////
* Ubosi nauhitaji, “koneksheni” iwapi / Vyeti vyangu sijafoji, gredi siyo makapi / Awezaye anihoji, ila mie simlipi / Maisha bila “konekti”, katu huwa hayaendi //// * Mgonjwa’ngu sipitali, “koneksheni” ya dokta / Yupo dhoofuli hali, matibabu hajapata / Asije kata kauli, yumkini tutajuta / Maisha bila “konekti”, katu huwa hayaendi ////
* Maji mie nahitaji, “koneksheni” ya fundi / Halali ama kufoji, mi nautaka ushindi / Menikifu ukosaji, nachochora kama bundi / Maisha bila “konekti”, katu huwa hayaendi ////
* Hapa nasema fakatu, nasaka koneksheni / Najongea nyatunyatu, wajuvi nijulisheni / Niipate hii kitu, inifae maishani / Maisha bila “konekti”, katu huwa hayaendi //// ** *
(Malenga ni Bin Omary)