Dunia tambala mbovu.
1 Yamenizonga mazonge, hakika nimenyongeka
Nimekuwa ni mnyonge, sipo kwalo watajika
Ukubwa wangu ni chenge, kila siku patashika
Dunia tambala bovu, upande wangu dekio
2 Likitoka hili lile, ni makubwa kwa madogo
Aina hizi na zile, yote yaniacha kodo
Kama kusali nasali, ila ningali ja sodo
Dunia tambala bovu, upande wangu dekio
3 Peke yangu naongea, naicheza ngoma goya
Nipo kati naelea, jama natamani koya
Mie nimeselelea, fuadini nina maya
Dunia tambaka bovu, upande wangu dekio
4 Au ninao upofu, s’oni jua ila giza
Natafuta uongofu, niweze ipata iza
Nina madeni sufufu, sio kama naigiza
Dunia tambala bovu, upande wangu dekio
5 Nafanya nyingi amali, yaisha makanyagio
Jana ndio afadhali, sioni matarajio
Uniondoke muhali, Rabi nipe mafikio
Dunia tambala bovu, upande wangu dekio
Fafanuzi ::
Chenge :: msitu uliokatwa kisha kuunguzwa
Ngoma gaya :: fanya kitu kisicho faida
Koya :: kufurahi baada ya jambo kwenda sawa
Selelea :: kudoda/kudorora
Maya :: ghadhabu
Sufufu :: _mengi sana
Amali :: kazi
Muhali :: shida/matatizo
(Malenga ni Abuuabdillah)