Ushairi

Bado Ninakusubiri.

BADO NINAKUSUBIRI

‘Lipoenda Somalia, sasa mwaka umekwisha
Pete bado ‘mevalia, huku ‘kinipa motisha
Bado nakusubiria, kwa wingi wa tumaini

Macho ‘lilitumbulia, ndege yenu ‘lipopaa
Majonzi ‘linivamia, ‘kahisi nami kupaa
Bado nakusubiria, nimo kwenye anga tua

Simu ‘naponipigia, hunilenga machozii
Woga hunikumbatia, nihisipo risasii
Bado nakusubiria, wangu wa dhati mpenzi

Ulivyonisimulia, nakumbuka kama jana
Chozi hunitangulia, kupanguza nang’ang’ana
Bado nakusubiria, weye wangu mahabubu

Shaka huniparamia, nionapo runingani
Alshabab wameshambulia, majeshi yetu kambini
Bado nakusubiria, machweo hadi macheo

Penzi ‘melikumbatia, tangu ulipoondoka
Nami nalipigania, lisije kutuponyoka
Bado nakusubiria, sina budi mahabubu

Nami ‘takusimulia, upweke ‘livyonikaba
Pia ukizingatia, sina mama wala baba
Bado nakusubiria, hadi mwisho wa dahari

(Ustaadh Momanyi)

Show More

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button
Close
Close